Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amefunguka na kusema kuwa yule mtoto ambaye anaonekana kuwa na asili ya nchini China ambaye mama yake alikwenda kulalamika katika ofisi yake wiki iliyopita, serikali ya China imeonyesha nia ya kutaka kumtunza.

Makonda ameweka wazi hayo  April 14, 2018 na kusema kuwa ameanza kufanya mawasiliano na serikali ya China kupitia Ubalozi wao na kudai tayari wamekubali juu ya hilo na kusema endapo vipimo vikibainisha kuwa mtoto huyo ni mtoto wa raia wao basi watakuwa tayari kumuhudumia.

“Waliponipa taarifa zile niliamua kuwasiliana na ubalozi wa China na tukawapa taarifa na taarifa hizo tayari wameshatuma nchini kwao kwenye ile kampuni ambayo baba wa yule mtoto aliyekuwepo kwa hiyo tunafanya utaratibu wote inawezekana mzazi wake yupo hapa hapa nchini au nje, siyo huyo tu wengi wapo Oman kule yaani kuna wazazi wengi wa kiume wapo huko ila watoto wao wapo hapa Dar es Salaam. Kwa hiyo si kwamba tunawatafuta tu waliopo nje ya mikoa lakini hata hawa ambao wako nje ya nchi tunatumia Wizara yetu ya Mambo ya Nje kupitia kwa balozi zetu zilizopo huko” alisema Makonda

Makonda aliendelea kutoa ufafanuzi kuhusu mtoto ambaye inasemakana raia wa China ambaye mama yake aliibuka kwenye ofisi zake na kusema kwa sasa hana mawasiliano na baba wa mtoto huyo ambaye anadai aliondoka nchini baada ya vibali vyake kuisha.

“Kwa mazungumzo tuliyonayo ya awali na huo ubalozi wa China wamekubali kwamba endapo mtoto yule ikibainika wao kama nchi watakuwa na wajibu wa kumtunza kwa hiyo muda si mrefu yule mtoto naye maisha yake yanaweza kubadilika na kupata neema lakini sina maana kwamba Watanzania sasa wazae na wachina ili waendeleaa kupata huduma hapana, tubaki kwenye misingi yetu ya kukubaliana nani anakuoa kwa jinsi ambavyo unataka maisha yako ayaendeshe” alisisitiza Makonda