Mshambuliaji wa Kimataifa wa Yanga Donald Ngoma amefunguka mengi baada ya kipindi kirefu kupita akiwa kimya na mengi kuzungumzwa wakati akiwa nje ya uwanja kwa takribani nusu msimu kutokana na maumivu ya goti.

Akiongea kupitia mahoajiano na mtandao wa klabu hiyo Ngoma ameeleza jinsi ambavyo alikuwa anapata ugumu kuona mashabiki wanaongea vitu tofauti na uhalisia wakati yeye alikuwa akipata matibabu ili aweze kurejea na kucheza vyema.

”Wakati mwingine ni vigumu kujua vipi mtu mwingine anaamini kwenye hali uliyonayo, kwenye soka upo wakati mgumu mchezaji unaweza kuupitia”, hiyo ni sehemu tu ya machache ambayo Donald Ngoma ameyasema kupitia mahojiano hayo.

Ngoma ambaye ni raia wa Zimbabwe amekuwa akituhumiwa na mashabiki kuwa hana uzalendo na timu hiyo na amekuwa akitumia njia ya kuumwa kama sababu ya kutocheza wakati ni mzima kabisa.

Ngoma amerejea hivi karibuni baada ya daktari wa timu ya Yanga Edward Bavu kujiridhisha na hali ya goti la nyota huyo hivyo kumpa ruhusa ya kuanza kucheza baada ya kuwa nje tangu mwaka jana. Mahojiano kamili yanapatikana kwenye mtandao wa Yangatv.