Monalisa Kuipeleka Tuzo ya APA Bungeni Leo
Siku mbili baada ya msanii Yvonne Cherrie ‘Monalisa’, kuibuka msanii bora wa kike katika tuzo za African Prestigious Awards (APA), anatarajia kuipeleka tuzo hiyo Bungeni leo.

Utoaji wa tuzo hizo ulifanyika Aprili 14, mwaka huu Accra, nchini Ghana, ambapo lengo lake ni kutambua maendeleo na tija aliyonayo mtu kwenye nyanja za uongozi, biashara, sanaa na kadhalika.

Taarifa kutoka kwa mama yake, Susan Lewis’Natasha’ zimeiambia MCL Digital leo kwamba baada ya msanii huyo kutua leo asubuhi, kesho anatarajiwa kwenda mjini Dodoma kwa mwaliko wa kuipeleka tuzo hiyo bungeni.

Kwa upande wake Monalisa kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, amewashukuru watanzania kwa namna walivyoweza kumpigia kura.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Monalisa amesema” Tuzo ni ya kwenu, mmekuwa nami kwa zaidi ya miaka 19 ya kazi yangu ya Sanaa hamjaniacha mnaendelea kunifurahia nashukuru mno mno, ahsante kwa muda wako uliotumia kunipigia kura.

Katika kipengele hicho cha muigizaji bora wa Kike, Mona alikuwa akichuana na wasanii maarufu wa kimataifa akiwemo Lupita Nyong’o ambaye ni mwigizaji wa Hollywood mwenye asili ya Kenya na Jack Apia mwigizaji kutoka nchini Ghana.

Waigizaji wengine waliong’aa kwenye tuzo hizo mbali na Monalisa ni Vicent Kigosi’Ray’ aliyeshinda kipengele cha muigizaji bora wa kiume na Moise Hussein aliyeshinda kwenye kipengele cha mpiga picha bora barani Afrika kwa mwaka 2017.

Hata hivyo mchekeshaji maarufu, Omar Athuman’Mzee Majuto ‘aliyekuwa akiwania kipengele cha mchekeshaji bora bahati haikuwa yake.

Kutokana na ushindi huo, sasa Monalisa ndio mwigizaji bora wa kike Afrika kupitia tuzo hizo za (APA) mpaka hapo shindano hilo litakapofanyika tena.