Serikali inatarajia kutoa mafunzo ya taaluma ya ukaguzi wa viuatilifu kwa wataalamu 100 ili kuongeza wigo wa ukaguzi wa maduka  ya kuuza viuatilifu mikoani na kuchukua nafasi ya watumishi waliostaafu.

Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba  ameyasema hayo leo Mjini Dodoma alipokuwa akiongea na waandishi wa habari alipokuwa akitoa ufafanuzi kwa Umma juu ya changamoto zilizobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika juu ya uwepo wa viuatilifu ambavyo havijasajiliwa sokoni.

“Jambo hili limekuwa changamoto kubwa kutokana na kuwepo kwa uingizaji haramu wa viuatilifu hivyo kutokana na mipaka yetu kuwa mirefu na kushindwa kuweka vituo vya ukaguzi katika kila eneo,” alisema Dkt. Tizeba.

Amesema Wizara ya Kilimo itaendelea kushirikiana na vyombo vya usalama ili kukamata vyombo vya usafiri vinavyotumika kuingiza viuatilifu hivyo kinyume na utaratibu. Aidha Wizara inaendelea kuongeza vituo vya ukaguzi mipakani na kuweka wakaguzi waliosajiliwa zamani pia itatoa mafunzo kwa waajiri wapya katika kipindi cha Julai – Septemba 2018.

Vile vile amesema, Wizara imetoa mafunzo kwa wauzaji wa pembejeo zaidi ya 1200 na miongozo kwa wazalishaji mbogamboga zinazouza nje ya nchi katika maeneo ya Arusha, Mbeya na Tanga ili kuzingatia taratibu za masharti yanayotolewa na nchi kuendelea kusafirisha nje ya nchi bidhaa za kilimo kutokana na kuwa na viwango vinavyokubalika vya viuatilifu.

Wakati huohuo, Waziri wa  Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina amemsimamisha kazi Meneja wa Kitengo cha Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) Dkt. Milali Machuma kutokana na kushindwa kusimamia ipasavyo kitengo hicho ambapo taarifa ya CAG imebainisha madhaifu katika usimamizi wa hifadhi za bahari na maeneo tengefu.

“Ninamsimamisha kazi Meneja wa Kitengo cha Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) Dkt. Milali Machumu mara moja kwa kushindwa kusimamia ipasavyo kitengo hicho, pamoja na kumsimamisha kazi  pia atachunguzwa,” alisema Waziri Mpina.

Waziri Mpina, pia amevunja bodi ya wadhamani na kuisuka upya ambapo mwenyekiti wa sasa Prof. John Machiwa pamoja na wajumbe wengine 8.

Vilevile amemuagiza Katibu Mkuu wa Uvuvi katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuunda kamati ya uchunguzi kuhusu utendaji wa Meneja.

Katika mfululizo wa mawaziri kueleza utekelezaji wa Serikali kutokana na hoja za CAG, kesho itakuwa zamu ya Wizara za Elimu Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto.