Serikali kupitia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe, imesema inakusudia kumpeleka msanii Nandy polisi juu ya video yake ya utupu iliyovuja.

Akijibu swali la Mbunge wa Ulanga Goodluck Mlinga alilotaka ufafanuzi kuhusu watu maarufu wanaovunja maadili kwenye mitandao ya kijamii na kutoa lugha za matusi, Waziri Mwakyembe amesema wizara imeweka kanuni rasmi za kuweza kukabiliana na watu wanaovunja maadili hususan kwenye mitandao, ambapo tayari imempeleka mahakamani msanii mkubwa ambaye video zake za faragha zimevuja, na pia inakusudia kumpeleka polisi msanii wa kike Nandy.

“Tulitunga sheria toka mwaka 2010 lakini tulikosa kanuni, na sasa hivi tumeshaweka, na zimeshaanza kufanya kazi, jana tumempeleka mahakamani msaniii Diamond kwa video alizorusha, na pia Nandy itabidi apelekwe polisi kuhojiwa”, amesema Waziri Mwakyembe.

Waziri Mwakyembe ameendelea kwa kuwataka vijana kutotumia mitandao ya kijamii vibaya kwani mitandao sio kokoro ya kupeleka uchafu wowote, kwa kuwa nchi ina maadili na utamaduni wake na inapaswa kuulinda.