Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeidhinisha ombi la kuunganisha benki ya Twiga (Twiga Bancorp Ltd) na benki ya TPB (TPB Bank Plc) na kuwa benki moja kuanzia kesho tarehe 17 Mei 2018.

Benki hiyo itaitwa TPB Bank Plc, ametangaza Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Bernard Kibesse, Jumatano tarehe 16 Mei 2018 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Benki Kuu jijini Dar es Salaam.

BoT, ambayo ina mamlaka ya kusimamia mabenki na taasisi za fedha kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, ilichukua usimamizi wa Twiga Bancorp kutokana na benki hiyo kuwa na upungufu mkubwa wa mtaji.

Uamuzi huo wa kuziunganisha benki hizo ambazo zote zinamilikiwa kwa sehemu kubwa na Serikali ya Tanzania unahitimisha jukumu la BoT kusimamia uendeshaji wa benki ya Twiga tangu tarehe 28 Oktoba 2016.

“Muungano huu utaifanya Benki Kuu kusitisha usimamizi wa benki ya Twiga na mambo yote kuhusiana na benki hiyo yatafanywa na benki ya TPB kuanzia tarehe 17 Mei 2018,” alisema Naibu Gavana Dkt Kibesse katika taarifa yake kwa waandishi wa habari.

Alieleza kwamba Benki mpya ya TPB itakuwa na mtaji wa kutosha kama inavyotakiwa chini ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006. Aidha, uamuzi huo unamaanisha kwamba wateja, wafanyakazi, mali na madeni yote ya benki ya Twiga yatahamishiwa TPB Bank Plc.

Dkt. Kibesse alisema uamuzi wa kuidhinisha kuziunganisha benki hizo umechukuliwa ili kuboresha uangalizi na utendaji wa benki zinazomilikiwa na Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. “Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha,” alisema Dkt. Kibesse.