Alex Apoko ‘Ringtone’

UKIINGIA Nairobi, Kenya ukaulizia wasanii wanaoongoza kwa mkwanja ni wazi utaambiwa Akothee mwenye utajiri wa milioni 600 za Kenya (sawa na bilioni 13 za Kibongo), Jaguar mwenye milioni 350 za Kenya (sawa na bilioni 8), Nameless mwenye milioni 100 za Kenya(bilioni 2) pamoja na Size 8 mwenye 500,000 za Kenya (sawa na milioni 11).

Wakati listi ikieleweka ni hiyo, msanii wa nyimbo za Injili, ameibuka na kusema kuwa ana utajiri kuliko msanii yeyote wa Kenya. Akifanyiwa mahojiano na TV ya Citizen nchini Kenya, Ringtone alisema kwa sasa ana utajiri wa shilingi milioni 800 za Kenya (sawa na bilioni 18 za Kibongo).

Ukiweka kando utajiri huo, juzikati Ringtone alizungumzwa na vyombo vingi vya habari mara baada ya kutaka kumzawadia mjasiriamali, Zarina Hassan ‘Zari The Bosslady’ Range Rover Sport modeli ya 2017 yenye thamani ya shilingi milioni 30 za Kenya (sawa na milioni 674).

Lengo la Ringtone ni kutaka kumuoa Zari mara baada ya kujiridhisha kuwa ameachana na mzazi mwenzake ambaye ni msanii wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Ringtone ni nani?

Alizaliwa miaka 28 iliyopita katika Wilaya ya Kisii, Nairobi Kenya. Akiwa bado mchanga, mama yake alimtupa ‘soko la uswahilini’ mitaa ya Tom Mboya kwa kuwa baba yake alimkataa na alikuwa akifanya kazi maeneo hayo.

Hata hivyo alitokea bibi mmoja aliyemuokota na kuamua kumlea japokuwa alikuwa akiishi katika maisha ya kuuza pombe za kienyeji aina ya Chang’aa. Ringtone aliwahi kukaririwa akimuongelea baba yake kuwa; “Nikiwa na miaka mitano nilisikia baba yangu amefariki dunia kabla hata sijamuona. Sikuumia sana kwa kuwa sikuwa hata najua amefananaje.”

Baada ya miaka miwili kufariki kwa baba yake, bibi aliyekuwa akimlea naye alifariki hivyo kuchukuliwa na mjomba wake ambapo alikuwa akiishi maisha ya tabu. Kutokana na hali ya maisha, mjomba wake aliamua kumpeleka kwa shangazi yake napo hali ikawa ngumu zaidi na kuamua kutoroka akiwa na miaka 15.

Azamia Mombasa

Baada ya maisha kumpiga, alienda katika Fukwe za Mombasa akiwa na ndoto kuwa atapata mwanamke mtalii wa Kizungu ambaye ataweza kumuoa na kumtoa kimaisha.

Alishindwa kutimiza ndoto zake na mwisho wa siku, alipata mwanaume wa Kizungu ambaye alimkalisha na kumuambia ndoto yake kubwa ni kumuamini Mungu hivyo akapelekwa shule za dini na huko ndipo alipojifunza mengi kumjua Mungu kupitia nyimbo za Injili. Alifanikiwa kutoa nyimbo kadhaa na kupendwa ambapo alikuwa akifanya shoo nyingi mashuleni na kwenye klabu za usiku.

Aanza kushika pesa

Maisha yake ya kushika pesa yalianza 2006 alipomuazima rafiki yake kiasi cha shilingi 7,000 za Kenya (sawa na 157,000 za Kibongo) na kuanza kuzunguka katika shule za sekondari kuuza CD za nyimbo zake, enzi hizo alikuwa akitamba Ngoma ya Inabamba.

Baada ya miezi miwili akawa ametengeneza kiasi cha milioni 1.8 za Kenya (milioni 40 za Kibongo) na kuiwekeza katika biashara nyingine zikiwemo za kuuza vifaa mbalimbali vya hospitali.

Utajiri wake

Kupitia biashara, shoo na mauzo ya kazi za muziki, Ringtone ameweza kumiliki jumba la kifahari maeneo ya Karen, Nairobi lenye thamani ya shilingi milioni 50 za Kenya (bilioni 1), jumba hilo linatajwa kati ya majengo yenye thamani kubwa mjini humo likiwa na vyumba zaidi ya vitano, mabafu kadhaa, sehemu ya kuogelea, jiko la kisasa, ukumbi wa sinema, sehemu kubwa ya kupumzikia.

Anamiliki pia gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 lenye thamani ya milioni 15 za Kenya(milioni 330 za Kibongo), Nissan Patrol, Range Rover Vogue alilowekea jina lake kwa thamani ya shilingi milioni moja za Kenya (milioni 11 za Kibongo) Range hilo lina thamani ya milioni 10 za Kenya (milioni 224 za Kibongo). Pia anamiliki Ranger Rover Sport 2015.

Ataka kumuoa Zari

Safari ya Ringtone kutaka kumuoa Zari haikuanza juzi wala jana, staa huyu anayetamba na nyimbo nyingi zikiwemo Pamela, Talanta na Tenda Wema zinazopendwa zaidi na Rais Kenyatta wa Kenya, amekuwa akimzungumzia Zari mara kwa mara.Baada ya kusikia Diamond na Zari wameachana Februali 14 aliiambia Citizen TV;

“Niwe mkweli Zari ni mrembo na ni mjasiriamali. Kwa muda mrefu nimekuwa nikitafuta namba yake. Napenda awe rafiki yangu lakini kwa yote kama Mungu atanibariki awe mke wangu! Kwa nini lisiwezakane, sijaoa. Nimefanikiwa, nimebarikiwa, ni mrefu, mweusi na mzuri.

“Sijawahi kukutana na Zari lakini anaongelewa sana Uganda, Tanzania na Kenya kwa hiyo akija Kenya ataongelewa pia. Mimi nina hofu ya Mungu, najua jinsi ya kujali na kutomuingiza katika matatizo. Ninapomuona Zari najua atafanya vema na kuwa Mama wa Kanisa.”Alitupia picha mtandaoni akiwa na ngombe na kusema.

“Hawa ng’ombe wako katika ardhi yangu ya Karen. Mashabiki wangu wa Uganda wamenikumbusha kuwa marehemu Ivan Ssemwanga (aliyekuwa mume wa Zari) alilipa mahari ya ng’ombe 100 kumpata Zari kwa hiyo nitalipa 40.”

Zari amjibu

Hivi karibuni, Ringtone alivyosikia Zari atafanya ziara Nairobi, alimnunulia Range Rover Sport ili kumpatia ambapo jitihada hizo ziligonga mwamba baada ya kukataliwa.

“Hapana! Sihitaji hilo gari. Nikihitaji kuingia katika uhusiano naingia. Mwaka huu nahitaji kuwa peke yangu na kumjenga Zari mpya. Kama nikija kuingia katika uhusiano sitaki kuwa na mtu maarufu tena,” alisema Zari alipoulizwa juu ya Range hilo.