Rais Dkt. John Magufuli ameagiza kampuni tatu za mafuta ya kula kulipa asilimia 25 ya kodi baada ya kubaini matanki saba kati ya yaliyokaguliwa yana mafuta safi yanayofaa kwa ajili ya matumizi.

Dkt. Magufuli ametoa agizo hilo Mei 15, 2018 baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Salaam na kusema mbali na kulipa kodi kampuni hizo pia zitatozwa faini kwa kudanganya kuwa na mafuta ghafi wakati zikitambua kuwa ni masafi yanayofaa kutumika.

Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kupeleka Bungeni muswada kwa ajili ya kubadili sheria ya kodi ili wanaoingiza mafuta nchini watozwe kodi kubwa kulinda viwanda vya ndani.

Katika ukaguzi uliofanywa na taasisi za serikali, zikiwemo Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Shirika la Viwango Tanzania, TBS, kwa kuchukua sampuli katika matanki mbalimbali, ilibaini kuwapo matanki yenye mafuta safi na ghafi pamoja na malighafi ya kutengenezea sabuni.