WAKATI maandalizi ya mechi ya hisani ya mchezo wa soka utakaowakutanisha uwanjani, Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa katika Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji pamoja na mwanamuziki wa Bongo Fleva, Ally Saleh Kiba ikizidi kupamba moto, nyota hao wanatarajia kuchangia sekta ya elimu hapa nchini kiasi cha Sh milioni 50.

Samatta na Kiba wamefikia hatua hiyo baada ya kuguswa na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu hapa nchini na kuamua kushirikiana kwa pamoja kuchangia kiasi hicho cha fedha kupitia mchezo wa hisani wa soka utakaofanyika Juni 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.

Mechi hiyo, pia itashirikisha nyota mbalimbali kutoka hapa nchini wakiwemo pia Silvestar Mjuni ‘Mpoki’ na Lucas Mhavile ‘Joti’ ambapo tayari wameshapata majukumu ya kufanya kwa ajili ya mechi hiyo.

 

Joti ni msemaji wa timu inayoundwa na Samatta wakati Mpoki ni msemaji wa kikosi cha Ali Kiba.

mratibu wa mechi hiyo, Hussein Hembe alisema fedha zitakazopatikana kupitia viingilio hizo zitatumika kwa ajili ya kununulia vifaa vya elimu kama vile vitabu na kompyuta.

“Niwaombe tu Watanzania wenzetu mabibi na mabwana kujitokeza kwa wingi siku hiyo uwanjani kwa ajili ya kuja kuwaunga mkono Samatta na Kiba katika kufanikisha jambo hilo,” alisema Hembe