Baada ya jana Mohamed Salah kuumia kwenye mchezo wa Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Real Madrid na Liverpool, Daktari wa timu ya taifa ya Misri Dkt. Mohammed Abu Ola amesema nyota huyo ana nafasi kubwa ya kucheza Kombe la Dunia.

Dkt. Abu Ola amesema baada ya mchezo aliwasiliana na daktari wa timu ya Liverpool na kumweleza kuwa picha za mionzi (X-ray) zimeonesha bega la Salah limeteguka kwenye mfupa mdogo na matibabu yalianza haraka ili aweze kupona kwa wakati.

Kwa mujibu wa Dkt. Abu Ola na daktari wa Liverpool Salah atakuwepo kwenye fainali za Kombe la Dunia. Salah aliumizwa na mlinzi wa Real Madrid Sergio Ramos na kutolewa dakika ya 31 baada ya kushindwa kuendelea na mchezo ambapo timu hizo zilikuwa bado hazijafungana.

Baada ya Salah kutoka Real Madrid walifanikiwa kushinda kipindi cha pili kwa mabao 3-1 na kutwaa ubingwa wa 13 na wa taatu mfululizo chini ya kocha Zinedine Zidane ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo.

Mabao ya Real Madrid yalifungwa na Gareth Bale mawili na Karim Benzema moja huku bao pekee la Liverpool likifungwa na Sadio Mane ambaye naye atakuwa na timu yake ya taifa ya Senegal kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi.