Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete amempongeza Mwanamitindo wa Tanzania  Flaviana Matata anayefanyia shughuli zake kimataifa kwa kujitolea kujenga madarasa, mradi wa maji na kutoa vifaa vya kujifunzia katika Shule ya msingi Msinune iliyopo Bagamoyo.

Mh. Kikwete ametoa pongezi hizo pamoja na shukrani kwa mwanamitindo huyo ambapo amesema kwamba hayo ni matukio ambayo yanaacha alama na kutaka watu wengine kuiga mfano wake.

“Jitihada anazozifanya Flaviana kutusaidia Miundo mbinu na vifaa zinastahiki kuenziwa. Hii ndiyo maana ya Matukio yanayoacha Alama. Tuige mfano mzuri wake. Kiwangwa inakushukuru, Bagamoyo inakushukuru, Pwani inakishukuru, Tanzania inashukuru.  Flaviana wewe ni Mabadiliko ya ukweli,” Kikwete.

Pamoja na pongezi hizo kutoka kwa Mbunge Ridhiwani Flaviana ametoa ombi kwa kiongozi huyo “Asante sana, tuwekee nguvu tupate umeme please kabla ya kuanza ujenzi wa nyumba za walimu”.

Flaviana Matata Foundation wamekabidhi  mradi wa maji safi na salama wenye hifadhi ya maji ya lita 32,000 kwa matumizi ya wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Msinune ikiwa ni pamoja na kukamilisha ukarabati wa madarasa saba (7), ofisi za walimu mbili (2) na maktaba.