Klabu ya soka ya Azam FC ambayo jana imekamilisha usajili wa aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma, imerejesha shukrani kwa viongozi wa Yanga kwa kutoa ushirikiano na kufanikisha usajili huo.

Msemaji wa Azam FC Jaffar Idd Maganga, ameeleza kuwa viongozi wa Yanga wameonesha ukomavu mkubwa kwenye masuala ya michezo baada ya kubariki kwa asiliia zote uhamisho wa Ngoma kutoka kwenye klabu yao na kwenda Azam FC.

”Niwapongeze tu viongozi wa Yanga kwa kuweka wazi suala la usajili wa Ngoma kuwa walikuwa wamemalizana naye na taratibu zote zimefuatwa, ni jambo la kiungwana sana ambapo hata sisi tuliwahi kufanya hivyo kwenye usajili wa Gadiel Michael”, amesema.

Mbali na hilo Azam FC pia imeweka wazi kuwa usajili wa Ngoma ni mwanzo tu ila mashabiki wasubiri masika ya usajili yanayokuja ambapo timu yao itakuwa tishio msimu ujao wa 2018/19.

Azam FC kesho usiku itakuwa mwenyeji wa Yanga kwenye mchezo wa ligi kuu soka Tanzania Bara, ambao utakuwa ni wa kufunga pazia la ligi msimu huu huku pia timu hizo zikiwania nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu.