Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema kwamba kutokana na nidhamu na utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano imepelekea watumishi wa sekta ya ardhi kubadilika na kuacha tabia ya kuendekeza rushwa kwa wananchi.

Lukuvi amesema hayo leo Mei 29, 2018 Bungeni Jijini Dodoma wakati wa kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/219 amesema kwamba watendaji wa ardhi kwa sasa hawana tena tabia ya kuendekeza rushwa na ndiyo sababu kubwa ya kupungua kwa migogoro ya ardhi.

“Wataalamu wangu walikuwa wanakula bila kunawa, sasa hivi wanawa mara tatu, kama kula wanakula kistaarabu, na ndiyo maana kero hazizalishwi sana, lakini pia kutokana na nidhamu iliyowekwa na Serikali ya awamu ya tano ya utendaji, watendaji wangu kidogo wamebadirika, yale waliokuwa wanafanya zamani sasa hivi hawawezi kufanya tena”, amesema Lukuvi.

Lukuvi ameongeza kuwa kwa watendaji wa ardhi ambao bado wanaendekeza rushwa watashughulikiwa na Wizara yake “Watendaji wote ambao bado wanaendekeza kero na migogoro ya rushwa, sasa dawa yake imepatikana kwasababu wote watakuwa chini ya Wizara moja hawatakuwa na kichaka cha TAMISEMI kwasababu kule walikuwa wanauwezo wa kukubaliana na madiwani, wizarani hatuna madiwani sisi ni sauti moja”

Kwa upande mwingine Waziri Lukuvi alitoa wito kwa watanzania kujenga tabia ya kulipa kodi ya ardhi mapema kila mwaka bila kusukumwa na serikali.

Akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Waziri Lukuvi ameomba wabunge kuizinisha kiasi cha shilingi bilioni 73.07 kwa matumizi ya miradi ya mendeleo na matumizi ya kawaida.