Spika Ndugai Ametoa Agizo Jingine la Kufanyika Uchunguzi

Spika Job Ndugai ametoa agizo jingine la kufanyika uchunguzi; ni kuhusu mwanamke aliyejifungua akiwa mikononi mwa polisi mkoani Morogoro.

Huo ni mwendelezo wa maagizo ambayo amekuwa akitoa kiongozi huyo wa chombo hicho cha kutunga sheria tangu kuanza kwa mkutano wa Bunge la Bajeti, Aprili 3.

Jana, Ndugai aliiagiza Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kufuatilia tukio la Amina Rafael kujifungulia nje ya Kituo cha Polisi cha Mang’ula mkoani Morogoro, akisisitiza kuwa Bunge lingependa kujua kuhusu upelelezi wa jambo hilo.

Mwanamke huyo alikamatwa badala ya mumewe aliyekuwa akisakwa na polisi kwa tuhuma za kununua kitanda cha wizi. Aliwekwa mahabusu kwa saa 10 na alipoanza kusikia uchungu, aliwataarifu polisi, lakini hawakumsikiliza.

Kwa mujibu wa Amina, alipozidi kumsihi polisi aliyetambulika kwa jina moja la Sele, hakutaka kumsikiliza na badala yake akampeleka nje ambako alikaa kwenye majani akiwa na uchungu hadi alipojifungua.

Wizara imeshaahidi kuchunguza tukio hilo, lakini hilo halikumtuliza mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lujualikali, ambaye jana aliomba mwongozo wa Spika kuhusu tukio hilo na Spika aliendeleza mwenendo wake ambao amekuwa akiuonyesha katika siku za karibuni.

Wiki iliyopita, Ndugai aliitaka Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuihoji menejimenti na bodi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusu madai ya mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga kuwa BoT inatumia fedha nyingi kuliko taasisi nyingine za Serikali kugharamia matibabu ya watumishi wake nje ya nchi.

Mlinga alisema matumizi yao yamepanda kutoka Sh1 bilioni na sasa wanatumia Sh12 bilioni kwa kuwa hawataki kutumia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Ndugai pia aliitaka Wizara ya Fedha na Mipango kujitathmini na kutoa fedha za korosho ghafi za wakulima ambazo wanapaswa kuzipata kwa mujibu wa sheria na sio hadi ‘walambwelambwe’.

Alisema suala hilo analipeleka kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kama hataona tija yoyote, atalirejesha bungeni.

Alikuwa ahitimisha hoja ya mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye aliyetaka Bunge kuahirisha shughuli zake kujadili jambo hilo aliloliita la dharura.

Ilivyokuwa jana

Katika kikao cha jana, Ndugai aliitaka kamati hiyo inayoongozwa na Mussa Azzan Zungu kufuatilia tukio la Amina na kulieleza Bunge watakachokibaini.

Katika maombi yake ya mwongozo, Lijualikali alisema kuna mikakati inafanyika kuficha ukweli wa tukio hilo.

Akiomba mwongozo huo, Lijualikali alisema maelezo yaliyotolewa bungeni Juni 8 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ambaye alionyesha kusikitishwa na suala hilo, na yale yaliyotolewa na ofisi ya kamanda huyo yanatia shaka kama kweli haki itatendeka.

“Juni 8, Naibu Waziri Masauni alilaani lile tukio na alikiri msichana yule kujifungua nje ya kituo, ila siku hiyohiyo ofisi ya RPC Morogoro ilitoa kauli kwamba Amina hakujifungulia polisi,” alisema Lijualikali.

“Kwa kuzingatia Waziri wa Mambo ya Ndani (Dk Mwigulu Nchemba) alisema inafanya uchunguzi na wamefungua jalada la uchunguzi na ofisi ya RPC imekana, nina shaka na hili.

“Ninaomba ikiwezekana Amina aitwe katika Kamati ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje aje ahojiwe ili tupate ukweli na tukiacha taarifa hizi za RPC zitaharibu uchunguzi.”

Baada ya Lijualikali kumaliza kuomba mwongozo, Spika Job Ndugai alisema: “Hili ni jambo ambalo (mbunge wa Arumeru Mashariki-Chadema, Joshua) Nassari aliliuliza na naibu waziri kulitolea maelezo. Sisi tushukuru tu Waziri wa Mambo ya Ndani yupo hapa. Tulipe muda.

“Itafika siku tutapenda kujua majibu ya upelelezi huo. Hakuna anayetaka kujenga misingi ya polisi wetu kufanya ukatili kwa kina mama wajawazito.

“Tuvute muda tu. Ni jambo la simanzi, wafanye kazi na askari wana taratibu zao na wanachunguza na wana namna yao ya kushughulika. Kamati ya Mambo ya Nje ya Zungu huko mbele, mkija mtupatie taarifa ‘what happened (nini kimetokea).”

Katika viwanja vya Bunge, Mwananchi lilizungumza na Mwigulu kuhusu kilichoelezwa na Lijualikali na akasisitiza kuwa anafuatilia suala hilo na “nikipata taarifa za kina nitawajulisha”.

Juni 8, Nassari aliliomba Bunge kujadili suala hilo kwa dharura akisema ni moja ya matukio yanayoendelea kujitokeza, ikiwamo Dar es Salaam na Mwanza na hatua hazionekani kuchukuliwa na mwenyekiti wa kikao hicho, Andrew Chenge kumtaka Waziri Masauni kutoa ufafanuzi wa suala hilo.

“Kwa niaba ya Serikali tunasikitika kwa kweli kwa tukio lile na jambo hili limefunguliwa jalada la uchunguzi,” alisema Masauni.

Alisema kulikuwa na tukio la wizi lililomhusisha mume wa Amina aliyetuhumiwa kuwa alinunua vitu vya wizi vilivyokutwa nyumbani kwake.

“Polisi walimtaarifu mama, kwamba atakaporejea (mumewe)afike polisi. Lakini hakufika na polisi walimchukua yule mama kwenda kumhoji,” alisema Masauni.

“Busara ingeweza kutumika hasa kutokana na hali yake. Wangemhoji na kumuachia kwa kujidhamini. Hali ya uchungu ilipomfika polisi, wakataka kumpeleka hospitalini na ndipo akajifungulia njiani karibu na kituo cha polisi.”

Tayari tukio hilo limelaaniwa na wadau tofauti wa masuala ya haki za akinamama wakitaka uchunguzi ufanyike kukomesha vitendo hivyo.
Chanzo :Mwananchi