Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeombwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kidunia wa viongozi wa vyama vya kisiasa ambayo yanafanyika huko nchini China.

Hayo yamewasilishwa na Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke wakati alipotembelea Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba kuonana na Ndg. Bashiru Ally Kakurwa, Katibu Mkuu wa CCM kwa lengo la kumpa pongezi za kuteuliwa na Mwenyekiti wa chama hicho Dkt. John Magufuli.

“Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC) kimeichagua Tanzania na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa mwenyeji wa mkutano huu mkubwa na wa kihistoria “CPC Dialogue with World Political Leaders in Africa”, amesema Bi. Wang Ke.

Pamoja na hayo, Bi. Wang Ke ameendelea kwa kusema “tunayo furaha na heshima kubwa kuwa na mkutano huo mkubwa Afrika na Tanzania kama sehemu ya mpango wa kuiunganisha dunia kwa barabara na usafiri wa maji ulioasisiwa na Ndg. Xi Jinping Katibu Mkuu wa CPC na Rais wa China”.

Kwa upande wake, Katibu Bashiru amemhakikishia Balozi Wang kwamba CCM kitaendeleza mahusiano ya kidugu na ya kihistoria kati ya CCM na CPC na nchi zetu mbili.

“Tunataka kujifunza zaidi kutoka China na hasa namna ya kujipanga kimkakati katika kushughulika na kuendeleza mapambano dhidi ya dhuluma na unyonyaji ili nchi yetu iinuke na kuleta manufaa makubwa kwa watu wetu wa Tanzania. Mwenyekiti wa CCM na Rais Dkt. John Magufuli anayo kazi ya kujenga uchumi utakaowezesha kujitegemea, uchumi wa kitaifa, uchumi utakaowaondoa watanzania kutoka katika maisha ya umasikini kama China”, amesema Bashiru.