Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dkt. Bashiru Ali amefunguka na kudai watanzania wanaitegemea Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa ndicho chombo imara kinachoweza kutoa huduma kwa wanyonge.

Dkt. Bashiru ametoa kauli hiyo Juni 13, 2018 wakati alipokuwa anazungumza na wananchi wa Jiji la Dodoma waliofika kumlaki pamoja na wanachama wa CCM na viongozi na kusema amepewa dhamana kubwa na wana CCM ya kusimamia mageuzi makubwa ambayo yanakirejesha chama hicho kwa wanachama na katika misingi ambayo iliasisiwa na chama hicho.

“Kuna umuhimu wa kuimarisha Chama Cha Mapinduzi, kwa sababu mambo haya ya mageuzi yanahitaji chombo cha uongozi, huwezi ukajenga uchumi wa kitaifa bila chombo cha uongozi, huwezi ukapambana na ufisadi, ukaimarisha uwajibikaji na uwazi ukatoa huduma za kijamii kwa wanyonge bila ya kuwa na chombo imara na chombo imara”, amesema Dkt. Bashiru.

Pamoja na hayo, Dkt. Bashiru ameendelea kwa kusema “kinachotegemewa na watanzania ni Chama Cha Mapinduzi na katika Ilani yetu ya uchaguzi kuna sura mahususi inayohusu uimarishaji wa chama chetu”.

Kwa upande mwingine,  Dkt.  Bashiru amedai hali ya maslahi ya watumishi wa chama hicho sio wa  kuridhisha huku akiwataka watumishi wa CCM kuendelea kufanyakazi kwa moyo wa kujitolea.