YOTE yanawezekana ukiweka nia! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia kauli aliyoitoa msanii wa muziki, Zuwena Mohammed ‘Shilole’ kuwa anatarajia kuachana na masuala ya muziki na kumgeukia Mungu wake kama alivyofanya Mzee Yusuf.

Shilole aliyasema hayo alipokuwa amealikwa kwenye futari ya msanii wa filamu, Irene Uwoya ambapo wakati akizungumzia mabadiliko yake katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan aliweka wazi kuwa, hana muda mrefu ataupiga chini muziki.

“Si unaona nilivyopendeza na vazi hili la kiislam? Basi kwa taarifa yako sina muda mrefu na mimi nitaacha muziki kama alivyofanya Mzee Yusuf, inawezekana kabisa, ni suala la kuamua tu.

“Kizuri ni kwamba nina vyanzo vingine vya kipato, si unajua nina ule mgahawa wangu pamoja na biashara zangu nyingine? Hizo zitanifanya niendelee kuishi nitakapokuwa nimechukua uamuzi huo,” alisema Shilole.