Serikali imesema Pato halisi la Taifa limeongezeka kutoka Shilingi trilioni 47.1 mwaka 2016 mpaka Shilingi trilioni 50.5 mwaka 2017.

Hayo yamesemwa leo bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango wakati akieleza mwenendo wa uchumi kwa mwaka 2017 huku akibainisha kuwa pato la kila mwananchi limeongezeka.

” Kutokana na kuimarika kwa pato la taifa, hata pato la mtu mmoja mmoja nalo limeimarika na pato la kila mwananchi limeongezeka kutoka Shilingi milioni 2.1 mwaka 2016 mpaka Shilingi milioni 2.3 kwa mwaka,” amesema Waziri Mpango.

Dkt. Mpango amebainisha kuwa sekta zilizochangia kuimarika kwa pato hilo ni uchimbaji madini na mawe iliyokua kwa asilimia 17.5, uchukuzi na usafirishaji mizigo asilimia 16.6 na habari na mawasiliano asilimia 14.7.