BADO msiba wa mtoto Patrick wa msanii wa filamu za Kibongo, Rose Alphonce ‘Muna Love’ haujasahaulika! Bado sarakasi zilizotokea katika msiba huo zinaendelea kutawala kila sehemu, jina la Muna linaweza kuwa limetajwa zaidi kuliko kipindi kingine chochote.

Huwa sipendi sana kuzungumzia mambo yaliyopita kwa sababu najua licha ya yote yaliyotokea, Muna ndiye aliyeguswa na kuumizwa sana na kifo cha mwanaye Patrick kuliko mtu mwingine yeyote.

Hata kama wapo ambao wataendelea kumzungumzia mabaya Muna, hilo haliondoi ukweli kwamba yeye ndiye aliyembeba Patrick miezi tisa kwenye tumbo lake, na yeye ndiye aliyeingia ‘leba’ pale Muhimbili wakati wa kumleta mtoto huyo duniani kwa hiyo anaelewa uchungu wake.

Hakuna binadamu aliyekamilika, kila mmoja hufanya makosa maishani mwake na yawezekana wapo ambao wanamuona Muna kama amekosea sana kwa kilichotokea wakati wao wana ‘dhambi’ zisizoelezeka.

Pigo alilolipata Muna linatosha kabisa kumfanya ajute sana ndani ya moyowake kama kuna makosa alikuwa akiyafanya kwa makusudi. Nawasihi watu wote wanaomtakia Muna mambo mabaya, waache ‘kumjaji’ sana kwamba ndiye aliyesababisha uzembe uliozaa mauti ya Patrick kwa sababu kama angekuwa na nia ya kumdhuru, pengine angefanya hivyo tangu akiwa tumboni mwake

Kama aliweza kumbeba tumboni mwake kwa miezi tisa na kumzaa kwa uchungu, kamwe hawezi kukubali kufanya uzembe ambao leo umesababisha mauti ya mtoto huyo! Tukubali tu kwamba wakati mwingine Mungu anakuwa na makusudi yake kuacha jambo fulani litokee, kwa hiyo mtoto ameondoka kwa mapenzi ya Mungu.

Hata hivyo, nimesikitika zaidi kupata habari za kuaminika kwamba licha ya haya yote yaliyotokea, eti Muna bado ana mpango wa kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kuzungumza nao kinagaubaga kuhusu mambo yote yaliyotokea.

Mshangao nilioupata baada ya kusikia haya, ni kama ule nilioupata baada ya Patrick kutangulia mbele za haki halafu muda mfupi baadaye mfiwa (Muna) akaporomosha ujumbe mreeefu Instagram akiwananga na ‘kuwachamba’ wabaya zake.

Unajiuliza, kama Muna asingeposti ule ujumbe siku ile, hizi drama zilizofuatia baada ya hapo zingetokea? Jibu ni jepesi kabisa, zisingetokea na huenda mambo yangefanyika kwa utaratibu, mtoto akazikwa kisha ndiyo drama zikaendelea.

Makosa yaleyale aliyoyafanya Muna na kusababisha taharuki kubwa kabla hata mwanaye hajazikwa, ndiyo yaleyale anayotaka kuyafanya leo kabla hata ya arobaini ya mwanaye.

Kama kweli Muna unao mpango wa kufanya hivyo, najua lengo lako kubwa litakuwa ni kujisafisha na kuelezea mabaya ya mzazi mwenzako, Peter. Sijui kama hulka hii ya ‘kushindana’ unayo siku zote au ni kwa sababu ya ‘kuvurugwa’ na msiba wa mwanao.

Waswahili wanasema funika kombe mwanaharamu apite! Yaliyotokea yameshatokea, usidhani unaweza kubadilisha chochote kwa kuzungumza na waandishi wa habari na kumwaga ugali kwa sababu tu Peter au Casto alimwaga mboga!

Hizo siyo hulka za wanawake wa Kitanzania, waliofundwa na kufundika kwa sababu mwisho wa yote, kila kitu kitapita lakini ile hatia ndani ya moyo wako itaendelea kukutafuna. Huwezi kujua Watanzania watayapokeaje unayotaka kuyasema, wanaweza kuamsha hata ambayo yalishapita.

Mshukuru Mungu kwa kilichotokea, ukitaka kulia lia na Mungu wako, usitegemee kupata huruma yoyote kwa walimwengu katika kipindi hiki. Onesha imani yako mpya ya wokovu kwa vitendo kwa kutolipa baya kwa baya na kuwasamehe wale waliokukosea saba mara sabini!