Habari ya mjini kwa sasa ni shepu ya Malkia wa Bongo Movie, Wema Sepetu.

Kila mtu anasema lake kuhusiana na shepu mpya ya Wema, ambapo kwa sasa anaonekana amepungua kwa kasi. Kwa sasa Wema sio bonge tena kama alivyokuwa zamani.

Ile shepu ya Wema ambayo alibeba nayo taji la Miss Tanzania mwaka 2006 ndio imeanza kurudi unaambiwa, japo haiwezi kuwa kama vile, lakini kidogo ameanza kuonekana.

Huko kwenye mitandao ya kijamii ambako Wema ana wafuasi wengi kwelikweli kama jeshi la siafu, ndio usiseme mambo ni moto na kambi kibao zinapambana kutemeana shombo. Wapo wanaosema Wema amefanyiwa upasuaji wa utumbo ikiwa ni mkakati wake wa kujipunguza huku wengine wakipinga.

Ishu ya kukatwa utumbo

Mei 29, mwaka huu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wema alishindwa kufika mahakamani hapo kuendelea na kesi inayomkabili huku ikielezwa kuwa yuko nje kwa matibabu.

Baadaye zikaibuka taarifa kuwa, Wema alikwenda nchini India na kufanyiwa upasuaji na utumbo wake umekatwa ili kupunguza unene. Pia, wengine wakadai kwamba, amefanyiwa upasuaji ili kumwezesha kupata mtoto.

Lakini, mwenyewe amefunguka. Kwanza amekiri alikwenda nje kwa matibabu lakini hajakatwa utumbo kama inavyodaiwa. Amesema alikwenda kwa ajili ya matibabu mengine tofauti ambayo hata hivyo hakupenda kutaja.

“Unajua nawaangalia tu wataalamu wa kuwasemea watu matatizo binafsi, sikwenda India kwa ajili ya kukatwa utumbo ili nipunguze unene. Kwanini nifikie hatua hiyo? Sina ustaa huo kabisa. Nilikwenda kwa matibabu yangu binafsi,” alisema Wema.