TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI BENKI KUU YA TANZANIA YACHUKUA USIMAMIZI WA BANK M TANZANIA PLC.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imechukua usimamizi wa benki ya M Tanzania PLC.

Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 02 Agosti, 2018 na BoT, ambayo iko hapo chini.

Ndugu Wanahabari, Kama mnavyofahamu, Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, imeipa Benki Kuu ya Tanzania mamlaka ya kusimamia shughuli zote za kibenki na taasisi za fedha nchini kwa lengo la kuhakikisha uimara na ustahimilivu wa sekta ya kibenki na kifedha kwa ujumla.

Napenda kuwataarifu kuwa, wa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha sheria namba 56(1)(g)(iii) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu ya Tanzania imeamua kuchukua usimamizi wa Bank M Tanzania Plc (Bank M) kuanzia leo tarehe 2 Agosti 2018.

Uamuzi huu umechukuliwa baada ya kubaini kuwa Bank M ina upungufu mkubwa wa ukwasi kinyume na matakwa ya sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake.

Upungufu huu wa ukwasi unahatarisha usalama wa sekta ya fedha na pia kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa Bank M kutahatarisha usalama wa amana za wateja wake. Ndugu Wanahabari, Kutokana na uamuzi huo, Benki Kuu imeisimamisha Bodi ya Wakurugenzi na uongozi wa Bank M kuanzia leo tarehe 2 Agosti 2018.

Kufuatia uamuzi 2 huo, Benki Kuu imemteua Meneja Msimamizi ambaye atakuwa na jukumu la kusimamia shughuli za Bank M kwa kipindi ambacho itakuwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu.

Aidha, umma unaarifiwa kuwa katika kipindi kisichozidi siku tisini (90) kuanzia siku ya taarifa hii, shughuli za utoaji wa huduma za kibenki za Bank M zitasimama ili kuipa nafasi Benki Kuu kutathmini hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa suala hili. Benki Kuu inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha.

BENKI KUU YA TANZANIA