Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla amepata ajali asubuhi hii akitokea mkoani Arusha kuelekea Manyara karibu na eneo la Magugu mkoani humo na mtu moja anadaiwa kupoteza maisha.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi (ACP) Agustino Senga amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo amesema, kwa sasa Dkt. Kigwangalla amekimbizwa katika kituo cha afya Magugu kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi kutokana na majeraha aliyoyapata.

“Ni kweli imetokea ajali hiyo na inadaiwa mtu mmoja ambaye ni mwandishi wa habari amefariki papo hapo, lakini bado sijapata jina lake kamili maana ndio nipo njiani naelekea eneo la tukio kwa sababu ajali imetokea muda si mrefu kutokea sasa. Mh. Kigwangalla, dereva wake pamoja na mlinzi wana majeraha na maumivu na sasa hivi wamepelekwa katika kituo cha afya Magugu kwaajili ya kupatiwa matibabu”, amesema Kamanda Senga.

Aidha, Kamanda Senga amesema kwa taarifa za awali chanzo cha ajali hiyo imesababishwa na mnyama ambaye alikuwa amekatiza ghafla barabarani na kusababisha gari aliyokuwa akitumia Waziri Kigwangalla kupoteza muelekeo na kusababisha ajali hiyo.