Hii Hapa Siri ya Jokate Kumpiku Irene Uwoya

WANAOWEWESEKEA uteuzi wa Miss Tanzania Namba 2, 2006, Jokate Mwegelo wameibua mapya, kwamba harakati za kusaka uongozi wa umma alizofanya mrembo huyo hazizidi zile za Miss Tanzania Namba 5 wa mwaka wake, Irene Uwoya, Ijumaa linakupa stori zaidi.

Hoja ya: “Kwa nini Jokate apewe ukuu wa wilaya; Uwoya aachwe?” ilishika kasi wiki hii mitaani na kwenye mitandao ya kijamii, siku chache baada ya Rais Dk. John Pombe Magufuli kuwateua baadhi ya wakuu wa mikoa, makatibu tawala na wakuu wa wilaya ambapo miss huyo alilamba dume.

Ilielezwa na wengi kwamba harakati za Uwoya, mrembo anayetoka katika kundi la vijana wa kike wasanii za kutaka kuwatumikia wananchi katika nafasi ya uongozi zina jasho jingi huku mfano ukiwa ni uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. “Uwoya anaushawishi mkubwa, aligombea Ubunge Viti Maalumu Umoja wa Vijana CCM (Chama Cha Mapinduzi) na kushinda kwa kishindo.

“Pamoja na mizengwe ya akina Munde (Tambwe mbunge viti maalumu Tabora wakati huo) na timu yake aliweza kushinda, hii inaonesha kwamba Uwoya siyo tu anajua siasa lakini ana uwezo mkubwa wa kuongoza na anakubalika katika jamii,” alisema Hussein Kambo mchambuzi wa masuala ya kisiasa aishiye Makumbusho jijini Dar.

RADO AJA NA LAKE KWA UWOYA

Wakati mambo ya uteuzi wa uongozi yakizidi kuwa moto msanii Simon Mwapagata ‘Rado’ yeye alikuja na lake kwa Uwoya, ambapo pamoja na kuusifu uwezo wake lakini aliuliza hivi:“Siamini kama ni kweli baadhi ya makada waliochaguliwa wamekushinda ama wamekuzidi elimu kiivyo.

“ …wewe ni mmoja kati ya wasanii mliojitoa kwa hali na mali kuipigania Serikali hii iliyopo madarakani, najua hujalalamika ila najiuliza tu ni kweli bwana Dogo Janja ana hadhi ya kuwa mume wa mheshimiwa?” Baada ya kuitupia posti hiyo kwenye mtandao wake wa Instagram amshaamsha ikakolea, mengi yakasemwa kujaribu kuwalinganisha kiuwezo Uwoya na Jokate.

IJUMAA LASAKA VYANZO

Kufuatia kuwepo na migongano ya hoja miongoni mwa wananchi wengi, Ijumaa liliamua kutafuta vyanzo makini ndani ya CCM chama ambacho mwenyekiti wake ni rais ambako pia Uwoya na Jokate walianzia huko kutafuta nafasi za uongozi wa umma ili kujua ukweli wa mambo kuhusu uwezo wa mamiss hao.

IJUMAA: Kaka hebu nidokeze kifupi tu, kumekuwa na kelele nyingi kuhusu uteuzi wa Jokate, mbichi ni hizi za Uwoya kuachwa licha ya kuonesha uwezo mkubwa katika kukitumikia chama.

CHANZO: Nakuomba tusizungumzie uteuzi, huu uko kwa rais; ukiniuliza mimi unakosea.

IJUMAA: Si uteuzi hasa, nisahihishe kidogo hapo kwamba unieleweshe kati ya Uwoya na Jokate nani amefanya vizuri katika harakati za kutafuta nafasi za uongozi kutoka ndani ya chama kinachoshika dola, maana wengine wanasema Uwoya amefanya vyema kuliko Jokate wanautaja uchaguzi wa 2015 ambapo Uwoya alishinda kura za maoni viti maalumu.

CHANZO: Ahaa! Ni kweli alishinda lakini siyo sababu ya kujivunia sana, kwenye siasa unavyomalizia ni muhimu zaidi ya ulivyoanzia.

UWOYA NA JOKATE WACHAMBULIWA

Chanzo kingine kutoka CCM ambacho hakikupenda kutajwa na kwamba kimefanya kazi za chama kwa ukaribu na mamiss hao kililiambia Ijumaa kwamba upo utofauti mkubwa kati ya warembo hao.

“Bahati nzuri watu wanajadili nafasi ya uteuzi wa rais jambo linalonirahisishia sana kazi ya kufafanua suala hili na kuweka utofauti wa Uwoya na Jokate.

“Hebu tujiulize tangu uchaguzi umemalizika Uwoya amefanya nini na Jokati amefanya nini kukisaidia chama.

“Tukimaliza hapo tuangalie warembo hao sifa zao kwenye jamii zikoje, tukijua hilo tutaacha kupigia kelele mambo ambayo hayana mashiko kabisa,”chanzo kilisema.

SIRI JOKATE KUMZIDI UWOYA ZAANIKWA

“Mimi nina mambo kama matano hivi naweza kuyaeleza kuhusu Uwoya, kwanza kabla ya kuyaweka wazi nikiri kabisa msichana huyu alipoamua kuingia kwenye siasa alifanya vizuri.

“Aliwavutia wengi na viongozi walimkubali hilo halina ubishi, ndiyo maana alifanikiwa hata kushinda kura za maoni, bahati mbaya kura za rais hazikukiwezesha chama chetu kupata viti maalumu vingi.

Uwoya alikuwa katika nafasi ya kumi bora, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipotoa nafasi CCM walipata viti maalumu 6, Uwoya akakosa nafasi, vinginevyo angekuwa mbunge leo; sasa ngoja nikupe tofauti za hawa wasichana.

Kwanza; nianze na hili lililoenea kwenye mitandao ya kijamii, nadhani umeliona la msichana huyu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na vijana, kidogo linapunguza sifa, mwenzake Jokate hajaonekana na hilo.

Pili; maadili yake siyo mazuri, vitendo vya kupigapiga picha za nusu utupu na kuposti kwenye mitandao ya kijamii ni mambo ya kijinga nalo linaondoa sifa ya mtu kuwa kiongozi, kwa Jokate hakuna tatizo kubwa.

Tatu; tuhuma za mambo ya kihuni Uwoya anazo mwenzake hana.

Nne; Uwoya hana uwezo wa kutunza siri, nakumbuka enzi zile za ugomvi na mume wake marehemu Ndikumana (Hamad Katauti) alikuwa akiposti kwenye mitandao hata mambo ya siri ya mumewe, hili nalo ni tatizo, sifa ya kiongozi haiko hivyo.

Tano; jambo kubwa la mwisho linalomtofautisha Uwoya na Jokate ni kuzikatia tamaa siasa. Alipokosa nafasi ya ubunge ni kama alisema hataki tena, akaendelea na mipango yake mingine.

Chanzo kiliongeza kuwa kwa Jokate haikuwa hivyo kwani hata alipoondolewa kwenye nafasi ya Naibu Katibu wa Itikadi na Uenezi Umoja wa Vijana CCM kitengo cha chipukizi, hakuacha siasa aliendelea kufanya kazi za jamii jambo ambalo anasema limemsaidia kuaminika.

UWOYA ASHAURIWA

Kiliongeza chanzo chetu: “Sasa haya machache nayajua mimi, lakini kumbuka vyombo vya usalama na washauri rais wana macho yao pia ya kuzingatia kwenye uteuzi wa mtu kuwa kiongozi wa umma.

“Mimi namshauri Uwoya kama mwanangu achangamke, ajitathimini, asikate tamaa vinginevyo ataichezea bahati na kila siku ataona wenzake wanapewa nafasi za kutumikia jamii yeye anaambulia kuweka picha zisizo na maadili mitandaoni.

“Sijui sinawasaidia nini hizi picha mbaya hawa watoto wetu, mimi sijui. Naomba wajifunze kwa wenzao vinginevyo ninyi vijana mna msemo wenu wa ‘watapata tabu sana’ na mimi nasema Uwoya asipobadilika atapata tabu sana.”

UWOYA AKIRI KOSA

Baada ya kuwekewa ujumbe mzito na Rado na baadaye kuchambuliwa vilivyo mitandaoni na baadhi ya watu Jumanne wiki hii Uwoya aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram kama ifutavyo kuonesha kukiri kwake kosa.

“Jokate amepambana na amekuwa karibu sana na harakati za chama na haswa kushiriki katika shughuli za kijamii kwa haya na mengi zaidi mimi nampongeza na kiukweli alipanda mbegu nzuri ambayo amevuna mavuno mazuri.

“Hongera sana kwa Mheshiwa Jokate Mwegelo. Na pia amini katika hili wakati wa MUNGU ni wakati sahihi zaidi na bado tuna muda na matumaini pia. Nitafanyia kazi pale nilipokosea na kurekebisha Asante.”