KATIBU MKUU wa Wizara ya Fedha na Mipango,  Bw. Doto James, amewaonya watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania – TRA wanaojihusisha na vitendo vya ukosefu wa maadili vinavyochangia kuikosesha serikali mapato yake yatokanayo na kodi, vikiwemo vitendo vya rushwa, kwamba watachukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.

Bw. James, ametoa kauli hiyo wakati akihitimisha kikao maalum kati ya Menejimenti ya Wizara ya Fedha na Mipango, Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Menejimenti pamoja na Mameneja wa Mikoa yote ya Tanzania Bara wa Mamlaka hiyo.

Amesema kuwa vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa Mamlaka hiyo ikiwemo vitisho kwa wafanyabiashara wakati wa kukusanya kodi havikubaliki na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kukabiliana navyo kwa nguvu zote.

Tayari wafanyakazi kadhaa wa Mamlaka hiyo wamefukuzwa kazi huku wengine wakihamishwa vituo vyao vya kazi kutokana na mwenendo wao usioridhisha na kulalamikiwa kutofuata maadili yao ya kazi wakati wanatekeleza majukumu yao.

Katibu Mkuu huyo ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kuhakikisha kuwa inafikia malengo ya kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 18 katika mwaka huu wa Fedha wa 2018/2019, ikiwa ni sehemu ya Bajeti ya shilingi trilioni 32.47, iliyopitishwa na Bunge ili kutekeleza majukumu mbalimbali ya Serikali ikiwemo miradi ya maendeleo.

Pause: Bw. Doto James – Katibu Mkuu-Wizara ya Fedha na Mipango

Kwa Upande wake, Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Bw. Adolf Ndunguru, amesema kuwa Mamlaka yake imefanyakazi kubwa ya kuongeza makusanyo ya kodi kutoka wastani wa shilingi bilioni 800 hadi kufikia shilingi trilioni 1.3 kwa mwezi.

Bw. Ndunguru amebainisha kuwa mafanikio mengine ni pamoja na kuongeza idadi ya walipakodi ikiwemo kuwasajili na kuwarasimisha wafanyabiashara ndogondogo walioko katika sekta isiyo rasmi ili waweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi.

Pause Bw. Adolf Ndunguru – Kaimu Kamishna – TRA

Ametaja baadhi ya changamoto zinazoikabili Mamlaka yake kuwa ni upungufu wa wafanyakazi, vitendeakazi yakiwemo magari, matumizi madogo ya mashine za EFD na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa na wadogo kukwepa kodi, jambo ambalo amesema wameanza kulikabili na hatua zake zimeanza kuzaa matunda.