Wizara ya Maliasili na Utalii imesema ipo mbioni kuanzisha Mamlaka ya Hifadhi za Fukwe nchini ili ziweze kusimamiwa ipasavyo kwa kujenga miundombinu bora itakayowavutia watalii wengi na  hatimaye kuongeza pato la taifa.

Hatua hiyo imekuja kufuatia agizo lililotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa alipokuwa  anawasilisha bungeni hotuba ya  makadirio ya mapato na matumizi ya fedha  kwa mwaka wa fedha 2018/2019 mjini Dodoma.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,  Japhet Hasunga  amebainisha hayo wakati alipotembelea Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Muingiliano wa Mto Ruvuma katika wilaya ya Mtwara vijijini  ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara ya kubainisha vivutio vya Utalii vilivyopo mikoa ya Kusini.

Amesema  Tanzania imejaliwa kuwa na fukwe nzuri lakini fukwe hizo zimekuwa zikitumika  visivyo baadala ya kutumika kama chanzo cha mapato kupitia watalii.

Amefafanu kuwa fukwe zilizo nyingi zipo tu na zimekuwa hazina uwekezaji wa namna yeyote ile wakati ni rasilimali muhimu sana katika kuongeza pato la taifa kwa vile watalii walio wengi kwa sasa  wameanza kuugeukia utalii fukwe baadala ya wanyamapori.

Akizungumzia hatua za awali ambazo Wizara inazifanya  kwa sasa, Naibu Waziri huyo amesema wameshaanza mazungumzo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo ndio Wizara inayozisimamia fukwe hizo kwa sasa.

Kwa upande wake, Kaimu Mhifadhi Mfawidhi Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Muingiliano ya Mto Ruvuma,  Jennifer Simbu amesema  mchakato wa kuunda Mamlaka hiyo uharakishwe ili Hifadhi hizo ziweze kuongeza   pato la taifa  kwa vile zitakuwa na uwezo wa kujitangaza

Aidha, Mhifadhi huyo Jennifer Simbu amesema mwaka 2010 kuna baadhi ya Wawekezaji walijitokeza wakitaka kuwekeza lakini hadi hivi sasa hakuna hata Mwekezaji hata mmoja kati ya watano waliopewa maeneo hakuna aliyeyaendeleza.