Mabingwa wa soka nchini England klabu ya Manchester City imetwaa ngao ya jamii nchini England kwa kuifunga Chelsea mabao 2-0 kwenye mchezo uliomalizika usiku huu kwenye uwanja wa Wembley.

Mabao ya Man City katika mchezo huo ambao umetoa baraka za kuanza kwa ligi kuu nchini humo msimu wa 2018/19 unaoanza Agosti 10, yamefungwa na Sergio Kun Aguero dakika za 13 na 58 na kushuhudia nyota huyo akiweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 200 ndani ya klabu hiyo.

Pamoja na kutwaa ubingwa huo, unaweza ukawa sio mzuri kwa kikosi cha Mhispania Pep Guardiola kuelekea kutetea ubingwa wao wa EPL, kutokana na rekodi yao kutokuwa nzuri kwenye ligi kuu msimu ambao wanakuwa wamechukua ngao ya jamii.

Manchester City walitwaa ngao ya jamii mwaka 1937 lakini msimu uliofuta wa 1937-38 walimaliza katika nafasi ya 21. Mwaka 1968 walichukua na msimu wa 1968-69 wakaishia nafasi ya 13.

Wakatwaa tena mwaka 1972 lakini msimu wa 1972-73 wakamaliza ligi wakiwa nafasi ya 11.  Mwaka 2012 wakachukua tena kwa kuwafunga Chelsea lakini wakamaliza ligi wakiwa wa pili. Je msimu huu itakuwaje ?

Katika mchezo wa leo ambao ulikuwa wa kwanza kwa kocha mpya wa Chelsea Maurizio Sarri, kwenye ardhi ya England, imeshuhudiwa kocha huyo akimwacha nje kiungo Jorginho ambaye walimgombania na Guardiola kwenye usajili kabla ya yeye kufanikiwa kupata sahihi yake.