Baada ya kikosi cha Simba kutua nchini usiku wa kuamkia leo Agosti 6, 2018, nahodha wa timu hiyo John Bocco na mshambuliaji Emmanuel Okwi, wamesema wanajivunia mbinu mpya kutoka kwa makocha wao wapya, kocha mkuu Patrick Aussems na kocha wa viungo Adel Zrane.

Akiongea mara baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, Bocco amesema utofauti wa kambi yao hauji kwa kuweka nje ya nchi bali ni kile walichokipata wakiwa Uturuki.

”Huko tumepata mbinu za ziada zaidi hususani kwenye eneo la mazoezi ya viungo, kocha wetu mpya kwa kutumia vifaa vya kisasa kwenye kambi tuliyokuwa tumefikia ametufundisha mambo mengi sana na kila kitu kimebadilika nadhani mtaona ligi ikianza”, alisema.

Kwa upande wake mfungaji bora wa timu hiyo msimu uliopita Mganda Emmanuel Okwi yeye amesema uwepo wa kocha mpya Mbelgiji Patrick Aussems, umewaongezea uwezo wa kushindana ambao watautumia kwenye mashindano mbalimbali wanayoshiriki msimu ujao ikiwemo ligi kuu na ligi ya mabingwa Afrika.

Simba inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Asante Kotoko siku ya Jumatano Agosti 8, kwenye tamasha lao la ‘Simba day’ ambalo huambatana na utambulisho wa wachezaji wapya pamoja na benchi la ufundi.