Uhamiaji Yatoa Sababu za Kuzuia 'Passport' ya Mkurugenzi wa Twaweza

Msemaji wa Idara ya Uhamiaji nchini, Ally Mtanda amesema kuwa wamezuia hati ya kusafiria ‘Passport’ ya Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Twaweza Aidan Eyakuze kwaajili ya kukamilisha taratibu za uchunguzi.

Mtanda amesema kuwa wamekuwa wakifanya hivyo mara kadhaa, pindi wanapopata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna mtu wana mashaka naye.

Mtanda amefunguka hayokuwa lengo la kushikilia hati ya Eyakuze sio kumzuia kutoka nje ya nchi kama watu wanavyodai lakini ni taratibu za Idara ya Uhamiaji na watakapokamilisha uchunguzi atafahamu hatma yake ikoje.

“Ni utaratibu wa kawaida unapotuhumiwa kuwa sio raia wa Tanzania, huwa Idara ya Uhamiaji tunazuia ‘passport’ kwakuwa ni mali ya Rais kwa maana hiyo ‘passport’ ni mali ya serikali, tukikamilisha uchunguzi ukagundulika ni Mtanzania basi utarejeshewa lakini ikiwa sio utafuata taratibu zingine wanazotakiwa kufanya raia wa kigeni”, amesema Mtanda.

Kuhusiana na suala la kumzuia kutumia hati ya dharura ya kusafiria, Mtanda amejibu kuwa, “hakutumia njia sahihi ya kuomba hati ya dharura kwakuwa tulivyoshikiria ‘passport’ yake alitakiwa kuja makao makuu kutoa taarifa, lakini yeye hakufanya hivyo alienda kuomba kibali katika ofisi zetu za wilaya bila kujua kuwa taarifa zake tayari zipo mipaka yote kuwa hatakiwi kutoka nje ya nchi, na alifanikiwa kupata lakini alizuiwa Airport baada ya taarifa zake kuonesha hatakiwi kutoka nje ya Tanzania”.

Agosti 3, katika mkutano wake na wanahabari, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze alitoa taarifa za kuzuiwa kutumia hati ya kusafiria ya dharura kwenda kuhudhuria mkutano wa kikazi jijini Kampala, baada ya Idara ya Uhamiaji kuzuia ‘passport’ yake.