Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Ally Salum Hapi jana amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali mkoani Iringa.
Katika mkutano huo Mhe. Hapi amewaelezea viongozi wa dini kama kundi muhimu katika jamii ambalo lina mchango mkubwa.

Hapi amewaomba viongozi hao kumpokea, kumuombea, kumpa ushirikiano na kumshauri pale inapobidi katika kuhakikisha anafanya kazi yake vizuri na kwa mafanikio mkoani Iringa.
Katika kikao hicho RC Hapi ameagiza kuundwa kwa kamati ya amani ya viongozi wa dini Mkoa wa Iringa jambo ambalo limekua kilio cha viongozi hao wa dini kwa muda mrefu.
“Mimi si mtu wa maneno. Kwa kuwa nanyi mmeitaka kamati hii muda mrefu, tutaiunda leo hii. Nitawaacha hapa mpendekeze majina ya kamati hiyo ili iundwe na kuanza kazi bila kuchelewa. Nami najitolea kuwa mlezi wa kamati.”
Alisema Hapi.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amepiga marufuku viongozi wa dini kusumbuliwa na kupangishwa foleni katika ofisi za serikali badala yake wapewe heshima na kipaumbele katika utoaji wa huduma.
Hapi ameagiza  wakuu wa wilaya kusimamia uundwaji  wa kamati za Amani katika wilaya zote za Iringa ili zifanye kazi kwa kushirikiana na kamati ya Mkoa, jamii na serikali kujenga umoja, amani na mshikamano katika kuijenga Iringa Mpya.
Viongozi wa dini waliohudhuria mkutano huo wamemshukuru Mkuu wa Mkoa na kumuhakikishia maombi, ushirikiano wa dhati huku wakipongeza kwa uamuzi wake wa kuwaheshimu na kukutana nao kama kundi la mwanzo katika uongozi wake.
Aidha wamemshukuru kwa uamuzi wake wa kuunda kamati ya amani ya Mkoa jambo walilolipogania kwa muda mrefu.
“Tunakushukuru kwa kutuheshimu na kututhamini sana Mkuu wetu wa Mkoa. Tutakuombea na tutakupa ushirikiano wote unaohitaji katika majukumu yako hapa Iringa,” alisema.
Katika ratiba aliyojipangia, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Ally Hapi anatarajiwa kukutana na wazee wa Mkoa wa Iringa kutoka katika wilaya zote za Mkoa huo siku ya jumamosi na kufanya nao mazungumzo.