Serikali yatishia kuzifutia leseni DStv, Zuku TV

MAMLAKA ya Mawasiliano (TCRA) imetishia kuzinyang’anya leseni kampuni za Multichoice Tanzania Limited na Simbanet Tanzania Limited kwa kukiukwa masharti ya leseni yao kurusha maudhui ya nje na kuitumia pia kuuza maudhui ya ndani kwa muundo wa malipo ya kabla (subscription).

Multichoice hurusha matangazo kupitia DStv ya Afrika Kusini, ambayo ni maarufu kwa chaneli mbalimbali za mpira na filamu.

Katika tangazo lake kwenye vyombo vya habari jana, TCRA ilieleza kuwa kampuni hizo hazina leseni ya kurusha maudhui ya ndani kama sehemu ya huduma zake.

“Mara kadhaa mamlaka imewataka kuzingatia masharti ya leseni kwa kutoweka maudhui ya ndani ambayo yana chaneli za bure, lakini yamekuwa yakiuzwa kinyume cha taratibu,” TCRA ilieleza katika tangazo hilo na kuongeza:

“Uchunguzi wetu (TCRA) umebaini kuwa kampuni hazifuati masharti ya leseni yake kwa kuweka chaneli za maudhui ya ndani kama sehemu ya huduma zake ambazo zinalipiwa.”

Mamlaka hiyo ilieleza zaidi kuwa licha ya kupewa amri na maelekezo mbalimbali kuhusiana na maudhui ya ndani kama sehemu ya masafa ya malipo ya kabla, bado wameendelea kutoa huduma hiyo ambayo haijaainishwa kwenye leseni yao.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, Multichoice Limited imevunja sheria kwa kubeba maudhui ya ndani na kulipisha wateja wake na kwamba hawaruhusiwi kuweka maudhui hayo kama sehemu ya huduma zao.

“Katika kutekeleza mamlaka yake, tunapenda kuujulisha umma kuwa wakati wowote tutasitisha leseni ya Multichoice kwa kushindwa kuendana na matakwa na kushindwa kuheshimu leseni na kuweka chaneli za maudhui ya ndani kama moja ya huduma zao,” ilielezwa katika tangazo hilo.TCRA pia ilisema kampuni ya Simbanet nayo itafutiwa leseni yake kwa kurusha maudhui ya ndani kama sehemu ya huduma zake za malipo ya kabla.

“Tangu Simbanet Tanzania Limited ivunje sheria kwa kutoa huduma ya maudhui ya ndani kwa malipo ya kabla kama sehemu ya huduma zake, katika kutekeleza mamlaka yetu (TCRA) tunaujulisha umma kuwa tunakusudia kusitisha leseni iliyotolewa kwao kwa kushindwa kufuata masharti yake ikiwamo kubeba maudhui ya ndani kupitia Zuku kama maudhui ya malipo ya kabla,” mamlaka hiyo ilieleza katika tangazo hilo.

Chaneli za ndani zisizopaswa kulipiwa ni ITV, Channel Ten, TBC, Star Tv na Clouds Tv.

Msemaji wa TCRA, Sem Mwakyanjala, alipotafutwa na Nipashe jana kutoa ufafanuzi juu ya tangazo hilo, alisema wamezipa mwezi mmoja kampuni hizo kuhakikisha zinatoa huduma kwa mujibu wa leseni zilizopewa.