Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo ameliagiza Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Biharamulo kuijadili taarifa ya uchunguzi ya upotevu wa mapato katika Halmashauri hiyo.

Uchunguzi huo umetokana na Kamati ya fedha ya Halmashauri hiyo kuunda timu ya uchunguzi ili kubaini upotevu katika ukusanyaji wa mapato.

 Waziri Jafo amefanya ziara hiyo leo Biharamulo akitokea Geita baada ya Halmashauri hiyo ya Biharamulo iliyopo mkoani Kagera Kushindwa kufikia malengo kwa kukusanya asilimia 60 huku kukiwa na taarifa za ubadhirifu wa mapato.

 “Kuna ubadhirifu wa kiwango kikubwa mpaka Kamati ya fedha ikaamua kuunda timu ya uchunguzi, niwaagize Baraza kukaa na kuwachukulia hatua watakaobainika kwenye hili ikiwa ni pamoja na kuwapeleka katika vyombo vya sheria,”amesema.

 Katika hatua nyingine, Waziri Jafo ametembelea Kituo cha Afya Nyakanazi ambacho kilipata Sh.Milioni 500 za ukarabati.

 Jafo ameridhishwa kwa kazi kubwa iliyofanywa kituoni hapo na kuwapongeza wananchi kwa ushirikiano wao uliowezesha kukamilika kwa miundombinu hiyo.

 Aidha Waziri Jafo ameendelea na ziara yake ya kikazi Mkoani Kigoma kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo.