NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amewashauri wakazi wa Wilaya ya Kakongo na mkoa wa Kigoma kwa ujumla kuchangamkia fursa za biashara kati ya mkoa huo na nchi jirani za Rwanda na Burundi kwa kuuza mazao ya kilimo  yaliyochakatwa likiwemo zao la muhogo ili waweze kunufaika na biashara hiyo ya mipakani.

Dkt. Kijaji ametoa rai hiyo mjini Kakonko baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa wilaya hiyo, mkutano uliolenga kujadili fursa na changamoto za ufanyaji biashara katika eneo hilo yakiwemo masuala ya kikodi.

“Nakuomba Mkuu wa Wialaya ya Kakonko uwakutanishe na kuwaunganisha wafanyabiashara hawa ambao nafurahi wengi wao ni vijana ili waandae andiko la namna ya kununua mashine za kuongeza thamani ya mazao ili wauze nje yakiwa yamechakatwa badala ya mfumo wa sasa ambao wanauza mazao ghafi nje ya nchi na hivyo kupata hasara” alisisitiza Dkt. Kijaji

Awali, wafanyabiashara wa Kakonko walimweleza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu kijaji, aliyeambatana na Kamishna wa Mapato ya ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. Elijah Mwandumbya, kwamba, bei ya zao la muhogo imeshuka kutoka shilingi 600 kwa kilo katika msimu uliopita hadi kufikia shilingi 150, hali iliyowasababishia wakulima maumivu makubwa.

“Wafanyabiashara wanaonunua mazao yetu kutoka Burundi ni watu wa kati kwa maana ya madalali ambao wananunua mazao yetu kwa bei nafuu na kuyapeleka n hini kwao ambako huyachakata na kuyauza kwa bei kubwa nchini mwao na nchi za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya kongo, hivyo tunaiomba Serikali itupatie mikopo kupitia Benki ys Kilimo ili tusnzishe viwanda vya kuchakata mazao yetu” alieleza mfanya biashara Dkt. Brighton Gwamagobe

Akizungumza katika Mkutano huo, Kamishna wa TRA wa Mapato ya Ndani Bw. Elijah Mwandumbya, pamoja na kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kodi, ametoa wito kwa wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari ili kuiwezesha Serikali kupata fedha za kuhudumia jamii ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya, maji na mambo mengine kadha wa kadha.

Alisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya ukusanyaji kodi na kutatua kero mbalimbali za wafanyabishara pamoja na kuongeza wigo wa walipa kodi ili kuimarisha mapato ya nchi

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, yuko katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma ambapo anakagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayopatiwa fedha na Serikali pamoja na kuzungumza na jumuiya ya wafanyabiashara.