Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewataka viongozi na maafisa waandamizi walioteuliwa kufanya kazi na Tume ya Madini iliyoanzishwa hivi karibuni kuwa mstari wa mbele kwenye mapambano dhidi ya rushwa kwenye maeneo ya kazi.

Naibu Waziri Nyongo aliyasema hayo leo tarehe 11 Agosti, 2018 alipokuwa akifunga mafunzo ya siku sita yaliyofanyika mjini Morogoro kwa kushirikisha viongozi na maafisa waandamizi walioteuliwa kufanya kazi na Tume ya Madini.

Alisema kuwa, mara baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo anatarajia kuona viongozi pamoja na maafisa madini wakazi wa mikoa na maafisa migodi wanakuwa vinara kwenye mapambano dhidi ya rushwa kwenye utoaji wa leseni na migodi.

Katika hatua nyingine, Nyongo aliwataka watumishi hao kufanya kazi kwa ubunifu hususan kwenye ukusanyaji wa maduhuli ili kuvuka lengo lililowekwa na Serikali.

“Ni matarajio yangu kuwa  kuanzia mwezi Septemba, mtaanza kukusanya maduhuli kwa njia ya kieletroniki ili kudhibiti upotevu wa fedha na kufikia lengo lililowekwa na Serikali,” alisema Naibu Waziri Nyongo.

Aliendelea kuwataka viongozi walioteuliwa kusimamia shughuli za madini mikoani kuhakikisha wanatatua migogoro  iliyopo kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji madini badala ya kusubiri viongozi wa ngazi za juu kutatua kupitia ziara mbalimbali wanazofanya kwenye maeneo hayo.

Awali akizungumza katika ufungaji wa mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila aliwapongeza viongozi na mafisa waandamizi walioteuliwa kufanya kazi na Tume ya Madini na kuwataka kuhakikisha wanafuata taratibu za makabidhiano ya ofisi kabla ya kuripoti kwenye vituo vipya vya kazi.

Mafunzo hayo yalilenga maeneo tofauti ikiwa ni pamoja na historia ya mabadiliko ya sheria ya madini, sheria ya madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017, muundo wa tume ya madini na mawasiliano ya ndani na nje ya tume.

Maeneo mengine ni pamoja na muundo na mfumo wa mawasiliano wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), taratibu za ofisi na makusanyo na maduhuli ya Serikali kwa njia ya kieletroniki (GEPG), usimamizi na utunzaji wa mali za umma, taratibu za utoaji wa leseni za shughuli za madini na ushirikishwaji wa wananchi/wazawa katika shughuli za madini.

Aidha maeneo mengine ni pamoja na ukaguzi wa madini na biashara, utatuzi wa migogoro katika sekta ya madini, taratibu za uwasilishaji wa taarifa makao makuu ya Tume na kwenye mamlaka nyingine zinazohusika, utunzaji wa siri katika utumishi wa umma, masuala ya utawala na rasilimaliwatu, sheria, kanuni na taratibu za fedha, usimamizi wa mifumo ya udhibiti wa ndani, maadili katika utumishi wa umma na mfumo wa uwazi wa upimaji utendaji kazi (OPRAS)