KAMPENI za udiwani kata ya Mawezi Manispaa ya Moshi zimehitimishwa leo huku Chama cha Mapinduzi (CCM) kikihitimisha kwa staili yake na Mbunge wa Kisarawe ambaye pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)Selemani Jafo kwa kujibu hoja moja moja jukwaani hali iliyowapa wakati mgumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) kutokana na hoja hizo ndio zilizokuwa tegemeo lao kwenye uombaji wa kura.

Hatua hiyo imewalazimu Vijana waendesha pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda na machinga wa Manispaa ya Moshi zaidi ya 42 kutoka Chadema kuhamia CCM katika dakika za mwisho baada ya kuridhishwa na majibu ya hoja yaliyotolewa.

Kampeni hizo hazikuwa na vijembe kama ilivyozoeleka badala yake zilikuwa za hoja nzito za utekelezaji wa Ilani ya CCM na mikakati ijayo kwa nchi pamoja na kata ya Mawezi kitendo kilichowavutia watu wengi kuacha kazi zao na kuja katika mkutano.

Miongoni mwa hoja zilizochambuliwa na Jafo ni pamoja na ujenzi wa kituo cha mabasi Moshi mjini, miundombinu ya barabara, Afya na Elimu.

Pamoja na Waziri Jafo wengine waliofanya upambanaji mkubwa jukwaani leo ni pamoja na Mbunge wa Siha Dk. Godwin Mollel na Mbunge viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro Ester Mmasi wakimnadi mgombea wa CCM Apaikunda Ayo Naburi.

Wabunge hao wamewaomba wananchi wa kata hiyo kesho kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kumpata Diwani atakayeongoza kata hiyo ya Mawezi ambayo ndicho Kitovu cha Manispaa ya Moshi.