Klabu ya soka ya Simba kupitia kwa msemaji wake Haji Manara imeweka wazi kuwa wanafuata nyayo za Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa kwa kuanza ujenzi wa uwanja wa Simba uliopo eneo la Bunju jijini Dar es salaam.

Haji Manara ameyasema hayo jioni ya leo kwenye uzinduzi wa uwanja wa soka wa Majaliwa unaojengwa wilayani Ruangwa mkoani Lindi ambapo timu ya Simba imecheza mechi ya kirafiki dhidi ya Namungo FC ya huko na kutoma suluhu.

”Kwakweli Waziri mkuu ameonesha mfano kwa viongozi na taasisi mbalimbai, sisi pia tunafuata haya mazuri aliyoyaanzisha na tunaanza ujenzi wa uwanja wetu Bunju mara moja ndani ya mwezi huu na ujao”, amesema.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua uwanja huo wa kisasa wa mpira wa miguu unaojengwa na halmashauri ya wilaya ya Ruangwa chini ya usimamizi wake na umeitwa jina lake ikiwa ni sehemu ya heshima kwake kutokana na kuanzisha mpango huo.

Majaliwa amesema suala la ujenzi wa uwanja ni jambo muhimu na hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linahamasisha ujenzi wa viwanja katika ngazi za mikoa na wilaya ili kutoa fursa kwa wananchi hususani vijana kushiriki katika michezo, hivyo amezitaka halmashauri nyingine ziige mfano wa wilaya ya Ruangwa.