YANGA itawasha mitambo yake kishikaji leo Jumapili mjini hapa kwa kuwatambulisha kwa mara ya kwanza wachezaji wao wapya saba kwenye mechi maalum ya kirafiki ya uzito mwepesi dhidi ya Mawenzi FC ndani ya Uwanja wa Jamhuri.

Kocha Mwinyi Zahera amesisitiza kwamba tayari timu yake imepata kikosi cha kwanza na leo atakitesti kwenye mechi hiyo itakayopigwa jioni kumuaga nahodha aliyestaafu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye ameitumikia Yanga kwa mafanikio.

Sura mpya saba zitakazotambulishwa leo ni pamoja na kipa Mkongomani, Klaus Kindoki, Deus Kaseke, Mrisho Ngassa, Jafary Mohammed, Mohammed Issa ‘Banka’ na straika Mkongomani Heritier Makambo.

Cannavaro kwa sasa atakuwa meneja mpya wa Yanga akichukua nafasi ya mwanachama mtiifu, Hafidh Saleh ambaye amepewa cheo cha uratibu, baada ya kudumu kwenye umeneja kwa miaka zaidi ya 10 mfululizo akiwa na makocha tofauti akiwemo Mkongomani wa mwisho kuinoa Yanga, Jean Bonghanya ambaye alitimuliwa na wanachama mazoezini.

Zahera ambaye pia ni Mkongo mwenye uraia wa Ufaransa anasema kwenye mazoezi aliyofanya Uwanja wa Highland Park mjini hapa, tayari ana kikosi cha kwanza lakini ni siri yake na hakitakuwa cha kudumu kwani kwake hakuna mchezaji mwenye namba kama haonyeshi juhudi.

Mchezo wa leo utakuwa wa kwanza kwa Yanga mpya kuonekana Morogoro mjini ambako ndiko watakakoanzia ligi msimu huu dhidi ya Mtibwa Agosti 23.