Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Kangi Lugola amesema kuwa kifo humkuta mtu wakati wowote na si kweli kila atakayepoteza maisha akiwa chini ya ulinzi wa vyombo vya dola anakuwa ameteswa na Jeshi la Polisi.

Mh. Lugola ametoa kauli hiyo Bungeni leo katika kipindi cha maswali na majibu wakati akijibu swali la Mbunge wa Konde (CUF) Khatib Said Haji lililohoji kuwa kuna tabia imeibuka hivi karibuni ya mahabusu kufia katika vituo vya Polisi na kusababisha ndugu kugoma kuchukua miili ya marehemu hao.

“Hivi karibuni kumekuea na matukio ya mahausu kufia katika vituo vya polisi, Je, ukiwa kama waziri mwenye dhamana unatoa kauli gani kukemea vitendo hivyo?,” alihoji mbunge Haji na kujibiwa na Mh. Lugola kwa kutumia vifungu vya biblia na kudai kuwa kifo kipo muda wowote na mahali popote na kutaka wananchi wasijichukulie maamuzi ya kuvamia vituo na kufanya fujo.

Waziri Lugola pia amekiri kwamba kumekuwa na matukio hayo siku za hivi karibuni ambapo wananchi wanafia mikono mwa polisi na pindi yanapojitokeza, wamekuwa wakifanya uchunguzi wa kina kama polisi wamehusika au la na kuchukua hatua.

“Mwananchi kufa huwa inatokea wakati wowote na mahali popote pale. Kwa hiyo mwananchi anaweza akafa akiwa polisi, anafanya mapenzi, akiwa safirini au hata humu ndani ya Bunge, ndio maana nimekuwa nikihoji huyu anayekufa akifanya mapenzi mbona hawaendi kuchoma kitanda na nyumba kwamba amefia mikononi mwa kitanda,” alihoji Mh. Lugola.

Mwanzoni mwa mwezi Agosti familia moja wilayani Temeke Jijini Dar es Salaam, iligoma kuuchukua mwili wa ndugu yao, Salum Kindamba, aliyefariki dunia Agosti 9, kutokana na utata wa ripoti iliyotolewa na hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kuhusu chanzo cha kifo chake wanachokihusisha na kupigwa risasi na polisi.