SHILINGI Bilioni tano zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa studio za Redio na Runinga za Shirika la Utangazaji Tanzania TBC katika makao makuu ya Nchi Dodoma.

Ujenzi huo ni mojawapo ya mpango wa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kuhamia Dodoma ambapo tayari wizara mbalimbali na maofisi ya umma akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wameshahamia.

Serikali kupitia Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu, Anthony Mavunde imesema kuwa inaendelea na jitihada za kupanua usikivu wa Shirika hilo katika mikoa na wilaya ambazo bado hazijwa na usikivu mzuri ambapo katika bajeti iliyopita kiasi cha Shilingi Bilioni moja kilitengwa kwa ajili ya kupanua usikivu wa mikoa ya mpakani.

Mavunde ameyasema hayo wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalumu, Anna Lupembe aliyeuliza ni lini Redio Tanzania itasikika katika kata za Ilela na Ilunde wilayani Mlele.

“Mkakati wa Serikali ni  kujenga mitambo ya redio katika mikoa ya Songwe,Katavi,Njombe na Simiyu katika bajeti ya mwaka 2019/20  na katika bajeti ya mwaka 2018/19 TBC imetengewa kiasi cha shilingi Bilioni tano kwa ajili ya kujenga studio za redio na luninga makao makuu ya nchi Dodoma”.Alisema Mhe. Mavunde.