Mtoto wa msanii mkongwe wa muziki wa dansi nchini Ali Choki, Junior Choki amefunguka na kukanusha  kwamba baba yake alizidiwa kiafya hadi kulazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza bali watu walizusha tu bila ya kuwa na uhakika.

Junior Choki amebainisha hayo alipokuwa anazungumza na eNewz inayorushwa na tinga namba moja kwa vijana ikiwa zimepita siku chache tokea kusambaa kwa taarifa zilizokuwa zimewashtua watu kuwa Ali Choki hali yake ni mbaya sana.

“Haikuwa hali mbaya sana kama ilivyokuwa imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa amelazwa ICU. Watu walivyokuwa wanachukulia ni tofauti alikuwa anaumwa kawaida tu na alilazwa wodini tu kama wagonjwa wengine”, amesema Junior Choki

Mbali na hilo, Junior Choki amewatoa wasiwasi mashabiki wa baba yake kuwa kwa sasa anaendelea vizuri kiafya na yupo nyumbani kwake mkoani Mwanza.

Ali Choki ni miongoni mwa wasanii wakongwe wa dansi walioweza kutamba nchini kupitia bendi ya Twanga Pepeta.