Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mh. Paul Makonda

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mh. Paul Makonda, amesema serikali ya mkoa wake, inapambana na matapeli wapya wanaotumia mbinu za kukopesha pesa watu au kuwarubuni wapenzi wao hususani wanawake na kisha kuchukua hati za nyumba zao na kuzitumia vibaya.

Makonda amebainisha hilo leo Septemba 15, 2018, wakati akiongea na wanahabari ofisini kwake, ambapo amesema pamoja na matapeli wanaokopesha pesa kwa hati lakini pia wapo wanaorubuni wapenzi wao au watu waliopo kwenye ndoa ili wawaibie hati za nyumba.

”Utapeli wa aina hii umezalisha kesi nyingi, kuna wasichana ambao wamerubuniwa na wapenzi wao wakaiba hati nyumbani na kuna wanawake wenye mahusiano nje ya ndoa zao nao wamerubuniwa wakaiba hati na zikaenda kutumika kukopa benki mwisho wa siku nyumba zikauzwa kufidia deni”, amesema.

Katika kutatua tatizo hilo Makonda amewaomba wananchi pamoja na benki kushirikiana na serikali ya mkoa, ili kuhakikisha matapeli wanakamatwa na pia kesi zilizopo mahakamani zinaisha kwa wakati ili wenye haki zao wapate.

Mapema mwaka huu, mkuu huyo wa mkoa alianzisha utaratibu wa kusikiliza kero mbalimbali za wananchi, zinazohitaji msaada wa kisheria, kupitia wanasheria ofisini kwake, ambapo ameeleza kubaini uwepo wa kesi nyingi za utapeli wa aina hiyo.

Pia amezitaka taasisi za fedha hususani benki, kujiridhisha na maelezo pamoja na ushahidi wa umiliki wa nyumba kwa watu wanaochukua mkopo kupitia hati. Ameeleza serikali ya mkoa haitasita kufuatilia haki za mwananchi hivyo benki zinaweza kupoteza fedha kwa kukopesha matapeli.