WAKATI msimu mpya wa michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania (FA) ikitarajiwa kuanza mwezi ujao, Shirikisho la soka Tanzania (TFF) limetangaza mfumo  mpya wa uendeshaji wa michuano hiyo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Salum Madadi, alisema kuwa tofauti na misimu iliyotangulia, safari hii mashindano hayo yatakuwa na mfumo mpya kwani yataanzia katika ngazi ya wilaya.

“Tumeelekeza mashindano haya sasa yaanze kwenye ngazi ya Wilaya, tumewapa majukumu vyama vya mpira vya mikoa, kuhakikisha wilaya zinacheza kupata bingwa, mabingwa hao wataenda kucheza ngazi ya mkoa na kumpata bingwa wa mkoa,” alisema Madadi.

Alisema kuwa mabingwa wa mikoa wataanza  kwenye awamu ya mwanzo ya kushindana ambapo watakaofanikiwa kupita hapo wataungana na timu za ligi daraja la pili, la kwanza na ligi kuu.

Alisema kwa mabadiliko hayo wanategemea mashindano ya mwaka huu  yatakuwa ni bora zaidi na yenye ushindani mkubwa kuliko msimu uliopita.

Timu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro ndio wanaoshikilia ubingwa wa michuano hiyo ulioutwaa Juni 2 mwaka huu kwa kuifunga Singida United mabao 3-2 kwenye mchezo wa fainali.

Mchezo huo wa fainali ulichezwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.