Naimani utakuwa unaniangalia Mzee Majuto- JB

Muigizaji mkongwe wa filamu nchini, Jacob Stephen ‘JB ameuomba radhi marehemu Amri Athuman maarufu King Majuto kwa kutoweza kuhudhuria katika kisomo chake huku akidai hatoacha kuzingatia yale aliyomuambia enzi za uhai wake.

JB ameeleza hayo kupitia ukurasa wake wa kijamii hii leo ikiwa ndio siku ya 40 tokea alipofariki na kuzikwa ambapo kwa waumini wa dini ya kiislamu huwa wanafanya kisomo cha kumuombea marehemu huko alipo

“Sikuweza kuungana nao leo Kama tulivyokuwa wote siku ya mazishi yako, lakini kama marehemu wanaona walio duniani naimani utakuwa ukiniangalia wakati naandika maneno haya na kuniambia usijali najua kwa hili hakika usingeweza kusafiri……

Bado sijaacha kukumbuka huwa naangalia picha zetu machozi yananitoka kama sasa, kisha na tabasamu na kusema dah King kifo hiki. Leo sio siku ya kulia ni siku ya kukuombea. Nimekuombea sana leo kwa imani yangu, sitaacha kukuombea nakumbuka maneno yako”, ameandika JB.

Mbali na hilo. JB amekiri maneno aliyowahi kuambiwa na marehemu Majuto kuwa kazi ya sanaa ni miongoni zilizokuwa na baraka kwasababu inaweza kuponya mioyo ya watu iliyokuwa na huzuni na simanzi.

“Ni kweli na nimeshuhudia, naimani bado utaendelea kukaa mioyoni mwa watu wengi na wataendelea kukuangalia kupitia kazi zako na kufurahi kila wanapokuwa na simanzi. Nakupenda sana na nafurahi ulikuwa unalijua hili. Endelea kupumzika kwa amani”, amesisitiza JB.

Marehemu Alhaji Amri Athuman ‘King Majuto’ alifariki dunia Agosti 8 2018 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alikuwa akipatiwa matibabu, kutokana na maradhi yake yaliyokuwa yanamsumbua.

Kifo cha Mzee wa Majuto kiliweza kugusa watu wengi kutoka ndani ya Tanzania na nje ya mipaka ya Tanzania, kutokana na uhodari na umahiri wa kazi za sanaa alizokuwa akizifanya na kukubalika kwa jamii yote kuanzia watoto hadi wazee.