Kaimu Rais wa klabu ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amefunguka na kuweka wazi kuwa Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Mrundi, Masoud Djuma, amekuwa hana maelewano na Mkuu wake, Mbelgiji, Patrick Aussems.

Abdallah amezungumza kupitia Azam TV akieleza kuwa ni kweli Djuma amekuwa hana mawasiliano mazuri na Aussems jambo ambalo limepelekea kuleta sintofahamu juu ya hatima ya kuendelea kusalia ndani ya timu hiyo.

Kaimu huyo amesema kuwa matatizo hayo yamekuwa yakijirudia tangu kipindi kile yupo Mfaransa Lechantre na wamekuwa wakijitahidi kuyarekebisha ili kuweka mambo sawa.

Hata Abdallah ameeleza kuwa hawezi kufukunyua kila kitu kwa sasa mpaka hapo baadaye kama klabu watakapokuja kuweka wazi mwafaka wa sakata hilo ili kusuluhisha kwa faida na maslahi mapana ya klabu.

“Ni kweli kumekuwa na matatizo ambayo yamekuwa yakijirudia baina ya Masoud Djuma na benchi la ufundi, haswa kwa makocha wakuu akiwemo Pierre Lechantre aliyeondoka. Tumekuwa tukifanya jitihada za kutatua tatizo hilo, siwezi kueleza mengi kwa sasa ila tutakuja na tamko rasmi baadaye”, alisema.