Mama mzazi wa aliyekuwa msanii wa Bongo movie Steven Kanumba, Bi. Flora Mtegoa, ameweka wazi sababu ya kukusudia kufanya filamu ya maisha ya Kanumba kuanzia utotoni hadi kuwa maarufu.

Mama Kanumba amesema kwamba mwanaye huyo ana maisha ambayo watu walikuwa hawayajui, maisha ambayo ana imani iwapo atafanikiwa kufanya filamu hiyo, atafikisha ujumbe mzito kwa jamii, hususani kina baba wanaokataa watoto.

“Kwanza ninataka kujulisha umma kwamba wanaume wasipende kukana watoto, ukizaa mtoto hata kama ni nje ya ndoa, lakini usimkane, mwambie rafiki yako au ndugu yako kwamba bwana wee, lolote linaweza likatokea, nina mtoto wangu moja, mbili tatu, usisubiri mtoto anakuwa mtu fulani ndio unajitokeza kusema fulani ni mtoto wangu”, amesema Mama Kanumba.

Mama Kanumba amesema suala hilo la kukataliwa ni moja ya maisha ya mtoto wake Kanumba, na ndio lililomsukuma kufanya filamu hiyo ambayo itakuwa na mengi yanayohusu maisha ya Steven Kanumba.