MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mkoa wa Arusha, umezitaka hospitali na vituo vya afya vinavyotoa huduma ya afya kupitia utaratibu wa malipo wa mfuko huo, kuwajali wagonjwa kwa kuwapatia dawa na huduma bora katika hospitali zao bila kuwabagua.

Akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja, Meneja wa NHIF Arusha, Isaya Shekifu, alisema kupitia wiki hiyo, ofisi yake ilitembelea hospitali mbalimbali jijini hapa zinazotibu wagonjwa wake kupitia bima hiyo na kugundua kuwapo kwa changamoto nyingi.

Alisema katika hospitali hizo walikutana na changamoto ya kuwapo kwa foleni kubwa ya wagonjwa wakisubiri kupata huduma jambo ambalo limekuwa ni kero kwa wagonjwa.

Aliongeza kuwa walikutana na changamoto ya kutokuwapo kwa dawa katika baadhi ya hospitali jambo ambalo limekuwa likiwalazimu wagonjwa kwenda kwenye maduka yanayotoa huduma ya dawa kupitia NHIF.

“Changamoto hizi pamoja na zingine nyingi tumezikuta kwenye hospitali zetu za serikali na binafsi, jambo ambalo siyo sawa kabisa kwa kuwa mgonjwa anapofika hospitali anatarajia kupata huduma zote muhimu, lakini kama anakosa huduma hizo na kulazimika kuzifuata mbali anakata tamaa,” alisema.

Alisema kama menejimenti ya mfuko watahakikisha wanakaa na watoa huduma katika hospitali hizo kuhakikisha changamoto hizo zinaondolewa na kuwapatia wagonjwa huduma nzuri zenye uhakika.

Kwa upande wake, Meneja Masoko wa NHIF Mkoa wa Arusha, Miradji Kisile, alisema kupitia wiki ya huduma kwa wateja waliweza pia kutembelea vituo vya watoto yatima wanaopata huduma za afya kupitia bima ya afya na kuwafariji pamoja na kugawa misaada mbalimbali.

“Mbali na hilo, pia tuliweza kuweka kituo kwa ajili ya kupima afya wateja wetu na wakazi wengine wa Arusha waliopenda kupata huduma hiyo hususani magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo kisukari na presha na kuwapatia ushauri wa namna bora ya kutunza afya zao,” alisema.

Alisema NHIF Kanda ya Arusha imekuwa ikitembelea wateja katika maeneo mbalimbali pamoja na kuendesha programu za kupima afya kwa wakazi wa maeneo tofauti ya Arusha mara kwa mara.