Jioni ya jana Oktoba 9, 2018, imeripotiwa taarifa ya kifo cha ‘Producer’ wa muziki nchini Tanzania Pancho Latino kutoka studio za B-Hitz ambaye amefariki kwa ajali ya maji.

Msanii Fid Q, ambaye ameweka wazi kuwa baada ya kupata taarifa za kifo alikwenda kuungana na watu waliokuwa na Pancho kwaajili ya taratibu zaidi.

”Ni kweli amefariki kwa ajali ya maji na kama unavyojua kifo chochote cha ajali kinakuwa kinahusisha polisi kwahiyo tumeripoti kituo cha Polisi Kawe kwaajili ya kupata kibali ili tuendelee na taratibu za Mochwari ambapo tumefanikiwa na sasa mwili wake tumeupeleka hospitali ya Lugalo” amesema Fid Q.

Fid Q amefafanua kuwa Pancho amefariki dunia jana jioni kwa kuzama baharini akiwa katika kisiwa cha Mbudya Dar es salaam hivyo kwa kuwa wameshatoa taarifa polisi taratibu zingine zitaendelea.

Amesema baada ya kumaliza taratibu za kuweka mwili Mochwari usiku huu, wanafanya taratibu za kukutana na familia yake ili kupanga zaidi kwaajili ya mazishi na ratiba zingine hivyo kufikia kesho wataeleza ratiba kamili.

Pancho amefanya kazi mbalimbali katika studio tofauti huku akidumu zaidi B-Hitz, ambako alitengeneza ngoma kama Dar es salaam Stand up ya Chid Benz, Bye bye Joh Makini, Ndege mtini Ferooz na nyinginezo.