Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewataka wadau wa maendeleo, viongozi wa dini, mila na watu mashuhuri nchini kuendeleza midahalo ya kimkakati ili kujadili athari hasi zitokanazo na ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni.

Naibu Waziri Ndugulile ameyasema hayo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike 2018 na kuhitimisha mdahalo maalum wa kitaifa uliofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 11 Oktoba, 2018  kuhusu kutokomeza mimba, ndoa za utotoni na ukeketaji.

Pamoja na changamoto husika zinazomkabili mtoto wa kike hapa nchini, Naibu Naibu Waziri Ndugulile ameagiza kuanzishwa na kuimarishwa kwa madawati ya ulinzi wa wanawake na watoto katika ngazi zote  na kuwasisitiza viongozi wa Mikoa na Halmashauri kuzingatia utekelezaji wa maagizo ya Serikali ambayo yametokana na maazimio ya washiriki kwani miongozo ya utekelezaji wake ipo.

Naobu Waziri huyo pia amewataka viongozi katika ngazi zote kuimarisha vituo vya mkono kwa mkono (one stop centres) kwa ajili ya kuboresha huduma kwa wahanga wa ukatili akifafanua kuwa vituo hivi vinapunguza mlolongo wa hatua za kutafuta msaada stahiki kwa kuhakikisha kuwa mhanga wa ukatili anapata huduma zote katika sehemu moja.

‘’Badala ya mtu kwenda kituo cha polisi kupata huduma na pia kuzunguka katika maeneo mengine kukamilisha taarifa muhimu ili tatizo lake liweze kufanyiwa kazi, uwepo wa vituo hivi vya huduma ya mkono kwa mkono mhanga wa ukatili anapata kila huduma katika kituo kimoja.”Alisisitiza Dkt. Ndugulile.

Aidha Naibu Waziri Ndugulile amesema yeye na Wizara yake pamoja na wadau wa maendeleo wataendelea kuihamasisha jamii kuendelea kutumia mitandao ya simu kwa ajili ya kutoa taarifa za ukatili dhidi ya watoto kwenye serikali za mitaa na kuhamasisha wanaume kushiriki katika kampeini za kutokomeza ukatili wa dhidi ya wanawake na watoto.

Wakati huo huo Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu katika hotuba yake kwa mgeni rasmi alitoa tathmini fupi ya mdahalo wa kitaifa kuhusu ukeketaji mimba na ndoa za utotoni na kusema kuwa kimsingi lazima tuunganishe jitihada zetu kuhakikisha tunakomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ili kujenga ustawi watoto.

Aidha Dkt. Jingu amezitaja mila mbaya ambazo zimekuwa zikiendeleza vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni kuwa mila potofu ambazo zimekuwa zikiendeleza maumivu ya kisaikolojia na msongo wa mawazo kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia.

Naye Mkuu wa Mahusiano ya Kimaendeleo wa Serikali ya Ireland Bi. Bronagh Carr amesema watoto wetu ni wazuri wawe wa kike au wa kiume lakini duniani kote watoto wa kike wanapitia katika kipindi kigumu ambacho kinakwaza maendeleo yao kielimu, mafunzo na ajira na kwa siku tatu za mdahalo tumesikia uhalisia wa yale yote yanayowakwaza wasichana.

Aidha Bi. Bronagh aliongeza kuwa uwekezaji kielimu kwa mtoto wa kike utavunja mzunguko wa ubaguzi na ukatili lakini pia ajila, ujasiliamali, ulinzi wa mtoto,utawala wa sheria, malezi na kuungwa mkono na familia pia vitapunguza ukatili wa kijinsia.

Mdahalo huo wa kutokomeza mimba na ndoa za utotoni pamoja na ukeketaji umeitimishwa leo kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike kwa mwaka 2018 ambayo imefanyika Kitaifa leo jijini Dar es Salaam.