Abdi Banda Afunguka Alivyokutana na Mkewe Zabibu Kiba "Nilimuomba Dada Yangu Aniunganishe Naye''

LEO tutakuwa na mwanasoka kutoka Tanzania anayechezea Timu ya Baroka ya Afrika Kusini; Abdi Banda, akisimulia namna ambavyo amekutana na mpenzi wake ambaye kwa sasa ni mkewe anayeishi naye Afrika kusini, Zabibu Kiba ambaye pia ni dada wa mkali wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba.
“Kiukweli nilikutana na mke wangu kipenzi Zabibu kupitia dada yangu, kwa kuwa alikuwa rafiki yake, nilimuomba dada yangu aniunganishe naye.
“Alifikisha ujumbe lakini hakuwa tayari kukubaliana naye, zilipita siku nyingi nikawa namsumbua dada yangu nikimueleza kuwa kiukweli nahitaji nimuoe. Nakumbuka ilifika kipindi nilirudi likizo nchini Tanzania, nikamuomba dada namba ya simu ya Zabibu kisha akanipa. Siku moja nikampigia kumueleza juu ya kile ambacho kipo moyoni mwangu juu yake.
“Lakini alinikatalia hapohapo na kuniambia huwa hawaelewi kabisa wacheza mpira na nafikiri alikuwa anahisi mimi namdanganya, isitoshe ni mtu ambaye amelelewa katika mazingira ya dini sana, hivyo haikuwa rahisi kwa kweli kiupande wangu lakini sikukata tamaa kwa kuwa nilikuwa nampenda kutoka moyoni.
“Nikarudi Afrika Kusini na Kuendelea na kazi yangu kama kawaida, tukawa tunawasiliana kujuliana hali, nikawa naendelea kumsisitiza kuwa namuomba anikubalie ili niweze kufunga naye ndoa maana umri wa kuoa kiupande wangu niliona kuwa umeshafikia.
“Nikaja kurudi tena Tanzania hatimaye tukaja kuonana na tukajikuta tunazoeana, tukaanza uhusiano na baadaye ikabidi tufuate taratibu za kifamilia. Nashukuru wazazi wake hawakuwa na kipingamizi.
Kwa kuwa ni jambo jema, hivyo nikafunga naye ndoa. “Sikutaka kumuacha Tanzania kwa kuwa nina maisha yangu Afrika Kusini, hivyo ikabidi niondoke naye. Nafurahi kwa kuwa ni binti ambaye anafuata maadili ya dini na pia ni muelewa kwa kuwa amekubaliana na mimi.
Hata nikisafiri kikazi huwa anabaki, na kwa kuwa maisha ya kule hayapo tofauti sana na alivyokuwa anaishi Tanzania. Kwa hiyo namuomba Mwenyezi Mungu anisaidie ili tuweze kuilinda ndoa yetu na atujaalie tuweze kupata familia yenye kufuata maadili ya dini,” alimaliza kusema Abdi Banda.