Inspekta wa Polisi Shabani Shabani kutoka kitengo cha Polisi mkoa wa Arusha akifundisha wanafunzi wa Shule ya Msingi Meru somo la Usalama Wetu Kwanza kabla ya mada kuu  ya madhara juu ya matumizi ya Madawa ya kulevya kwa wanafunzi.

 Jeshi la Polisi mkoani hapa kupitia kitengo cha Polisi Jamii ambacho kinaongozwa na Ofisa wa Polisi Mrakibu Msaidizi (ASP) Edith Makweli akisaidiana na wakaguzi wawili Shabani shabani na Marijani Mrope wameamua kufunga ofisi na kuwafuata wanafunzi shuleni kwa nia ya kufundisha Progarmu mbalimbali za Polisi Jamii ikiwemo Usalama Wetu Kwanza.

Mkuu huyo wa kitengo cha Polisi Jamii mkoa wa Arusha alisema kwamba wameamua kuwafuata wanafunzi shuleni na kuwafundisha vipindi mbalimbali juu ya Ulinzi Shirikishi lakini hasa wataendelea kujikita katika kutoa elimu juu ya madhara ya Madawa ya Kulevya.

(ASP) Edith alisema kwamba Jeshi hilo kupitia kitengo hicho limeamua kuanzisha mpango maalum wa utoaji elimu ili kukinusuru kizazi hicho kisijiingize kwenye dimbwi la watumiaji wa madawa ya kulevya hapo baadae.

Alisema Programu hiyo inayojulikana kwa jina la USALAMA WETU KWANZA imeanza kufundishwa juzi katika shule ya Msingi Naura na jana katika Shule ya Msingi Meru zote zipo ndani ya halmashauri ya jiji la Arusha na baadae kuendelea kutolewa kwenye shule nyingine za mkoa huu.

Katika mafundisho yaliyofanyika jana Shule ya Msingi Meru Maofisa hao waliambatana na Bw.Moses Chacha kutoka kituo cha Arusha Recovering Sobber House kilichopo Ngaramtoni ya Chini  ambaye awali alikuwa mwathirika wa dawa za kulevya na kwa sasa ni muelimishaji juu ya madhara ya madawa hayo.

Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii mkoa wa Arusha Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Edith Makweli akiwaelezea Wanafunzi wa Shule ya Msingi Meru namna kitengo hicho kilivyojipanga kuwanusuru wanafunzi ili wasijiingize katika matumizi ya Madawa ya kulevya

 Bw. Moses Chacha alisema kwamba ameamua kuungana na Jeshi la Polisi kupinga matumizi ya dawa za kulevya ili waelimishwaji wapate uhalisia wa mtu ambaye awali alikuwa mtumiaji wa madawa hayo.

Akitoa elimu juu ya madhara hayo kwa wanafunzi wa darasa la Nne na Tano katika Shule ya Msingi Meru alisema kwamba awali akiwa darasa la Kwanza alikuwa na ndoto ya kuwa rubani lakini ndoto yake ilifutika baada ya kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema katika safari ya maisha yake vitu vitatu ambavyo ni ULAZIMU, KUANGAZA NA UBINAFSI vimemgharimu na kuwaasa wanafunzi hao waviepuke na badala yake wawe wakweli, wafungue akili pindi wanapopokea taarifa na kuitafsiri kama ina uzuri au ubaya na kuwa na nia ya kufikia ndoto zao hasa kwa kufuata ushauri wa wazazi na walimu.

“Nilikuwa nawalazimisha wazazi wangu kupata kitu fulani lakini hiyo ilitokana na kukiona toka kwa wenzangu ili nikimiliki, sasa baada ya wazazi kushindwa kunitimizia nikaamua kujiingiza kwa marafiki ambao walikuwa na mahitaji niliyoyataka kisha kujiingiza kwenye utumiaji wa madawa”. Alifafanua Bw. Chacha.

Kwa upande wa Mwalimu Esther Mollel na Mwanafunzi wa darasa la Nne Abdul Kassimu ambao ni miongoni mwa waliohudhuria somo hilo walisema kwamba, wanalishukuru Jeshi la Polisi kwa kutoa elimu katika shule yao na kuwataka waendelee kuelimisha wanafunzi wa shule nyingine.

“Ni somo zuri limewajenga na kuwafungua ufahamu Wanafunzi wetu na hata mimi Mwalimu wao, tumejifunza kiuhalisia kwa kuwa tumemuona Mhanga na Polisi waendelee kutoa elimu hiyo kwa shule nyingine pamoja na kugawa vipeperushi ili visaidie kuwakumbusha wanafunzi.” Alisema Mwalimu Esther Mollel.

“Jeshi la Polisi liendelee kutoa elimu kama hiyo kwa Shule nyingine kwani kama alivyosema Mhanga watu wengi wamepoteza ndoto zao kutokana na kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya”. Alisema Abdul Kassimu Mwanafunzi wa darasa la Nne shule ya Msingi Meru.

Picha no.1. Inspekta wa Polisi Shabani Shabani kutoka kitengo cha Polisi mkoa wa Arusha akifundisha wanafunzi wa Shule ya Msingi Meru somo la Usalama Wetu Kwanza kabla ya mada kuu  ya madhara juu ya matumizi ya Madawa ya kulevya kwa wanafunzi. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)

Picha no.2. Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii mkoa wa Arusha Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Edith Makweli akiwaelezea Wanafunzi wa Shule ya Msingi Meru namna kitengo hicho kilivyojipanga kuwanusuru wanafunzi ili wasijiingize katika matumizi ya Madawa ya kulevya. (picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)

Mtoa elimu ya madhara juu ya matumizi ya dawa za kulevya Bw. Moses Chacha toka katika kituo cha Arusha Recovering Sobber House akipima uelewa wa wanafunzi kwa kuwachagua baada ya kuwauliza maswali yaliyotokana na mada aliyowafundisha juu ya madhara ya Madawa ya Kulevya (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)