Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Ally Mwalimu (Mb.) anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mwanamke Anayeishi kijijini itakayofanyika kwa mara ya kwanza kitaifa tarehe 15 Oktoba, 2018 mkoani Dodoma katika Halmashauri ya Chamwino, Kata ya Manchali, kijiji cha Manchali B. Aidha, maadhimisho hayo yanatarajia kuwaleta pamoja wanawake, wanaume, wasichana na wanaume wanaoishi kijijini wakiwemo watunga Sera, Asasi za Kiraia, wadau wa maendeleo na Taasisi Binafsi kwa lengo la kutafakari na kujadili kuhusu fursa na changamoto za Mwanamke anayeishi kijijini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Wizara inasema kuwa Madhumuni ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mwanamke Anayeishi Kijijini ni kuiwezesha jamii kutambua na kuthamini mchango wa kundi hilo hususan katika kuimarisha uchumi wa viwanda na maendeleo ya kilimo pamoja na kuchukua hatua za makusudi za kuboresha hali ya wanawake na wasichana wanaoishi vijijini.

Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa kupitia maadhimisho haya wanawake wanaoishi kijijini watapata nafasi ya kufahamu jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau mbalimbali na pia watapata fursa ya kutoa mrejesho wa namna ya kuboresha afua na huduma hizo.

Aidha Kaulimbiu ya Siku ya Kimataifa ya Mwanamke Anayeishi Kijijini inasema  ”Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Tuimarishe Miundombinu, Huduma za Jamii kwa Wanawake na Wasichana Wanaoishi Vijijini”. Kaulimbiu hii imezingatia vipaumbele vya kitaifa na muktadha wa nchi yetu na msisitizo mkubwa umewekwa katika kufikia uchumi wa viwanda na maendeleo ya watu hususan wanawake na wasichana wanaoishi vijijini kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na  Mpango wa Taifa wa Pili wa Maendeleo 2015/16 – 2020/21 pamoja na Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto 2016/17 – 2021/22.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa Wizara inawahimiza wanawake na wasichana hususan wanaoishi kijijini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho kwa kutafakari, kutathmini na kutumia ipasavyo fursa zinazotokana na jitihada za kimaendeleo zinazofanywa na Serikali na wadau mbalimbali ikiwemo uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, uboreshaji wa huduma za afya, uboreshaji wa miundombinu ya usafiri ikiwemo barabara kupitia Taasisi ya TARURA na uwezeshaji wa upatikanaji wa huduma za umeme vijijini kupitia  Taasisi ya REA.